Makandarasi wa ndani changamkieni fursa utekelezaji wa mradi wa TACTIC: Eng. Kanyenye

 

Makandarasi wazawa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuomba tenda mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya uboreshaji miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) ili kuweza kunufaika na fursa hiyo kama sehemu ya kukuza uchumi wa Tanzania na kuimarisha mzunguko wa fedha nchini.

Wito huo umetolewa leo Juni 02, 2025 mkoani Singida na Mratibu wa miradi ya Benki ya Dunia TARURA, Mhandisi Humphrey Kanyenye wakati wa utiaji saini wa miradi itakayohusisha ujenzi wa soko la Kimataifa la Vitunguu, ujenzi wa barabara za katikati ya Mji na Viwandani (Km 7.52) pamoja na ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wa Mnung'una, utakaokuwa na urefu wa Km 2.6 na jengo la usimamizi na uratibu wa miradi hiyo.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi mzawa M/s Sihotech Engeneering Company Limited kwa kushirikiana na kampuni ya AMJ Global Mult Contractors kwa gharama ya shilingi 24, 748,966,236.05 na ukitarajiwa kukamilika kipindi cha miezi kumi na tano kitakachoanza Juni mwaka huu.

"Maeneo mengi tumepata wakandarasi wa Kichina lakini kwa Manispaa ya Singida tumepata bahati ya kupata mkandarasi mzawa na yeye pia amefanya kazi maeneo mengine na katika kulinganisha utendaji kazi wake kulinganisha na wakandarasi wa Kichina, Mkandarasi huyu yupo mbele kwa asilimia zaidi ya 20,” amesema Mhandisi Kanyenye.

Mhandisi Kanyenye ameeleza kuwa, kukamilika kwa mradi wa TACTIC kutaleta manufaa makubwa kwa Manispaa ya Singida ikiwemo kuongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuboresha hali ya biashara katika maeneo husika, hivyo kuchangia maendeleo ya muda mrefu ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Soko la Kimataifa la Vitunguu litajengwa mkoani Singida likitarajiwa kuwa na jengo la ghorofa mbili likiwa na eneo la kuchambua vitunguu, kukaushia vitunguu, maduka 10, Vyumba 4 vya huduma za kifedha, pamoja na maeneo mengineyo likitarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri kutoka Milioni 300 hadi Milioni 505 litakapokamilika.



Chapisha Maoni

0 Maoni