WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha
wanaendelea kuhamasisha wananchi kutumia huduma ya kisheria ya Mama Samia ili
iwasaidie kutatua changamoto zao za kisheria.
Amesema kuwa juhudi
za utoaji haki haziwezi kufikiwa na Serikali pekee bali zinahitaji ushirikiano
wa dhati kutoka kwa kila mmoja ikiwemo viongozi, wazazi, jamii, taasisi za dini,
mashirika ya kiraia na wananchi kwa ujumla.
Amesema hayo leo
Jumatatu (Juni 16, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika ufunguzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika
Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika kwenye viwanja vya Maturubai Mbagala jijini
Dar es Salaam.
“Dhamira ya
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki kwa
wakati bila ubaguzi, ili kujenga jamii yenye mshikamano na utawala wa sheria,
Kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake, tunaweza kuwa Taifa linalojivunia mfumo
wa haki ulio imara, unaoaminika, na unaowalinda raia wote kwa usawa.”
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania
inaendelea kuwa Taifa linaloongozwa kwa kuzingatia haki, usawa na utawala wa
sheria kwa kuwa ndiyo msingi wa amani ya kweli na maendeleo ya kudumu.
Amesema kuwa wajibu
wa kila mtanzania, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wadau wa maendeleo
kushirikiana na Serikali kuhakikisha juhudi hizo zinaungwa mkono na zinaendelea
kuzaa matunda kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Pia, Mheshimiwa
Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kutoa taarifa za uwepo wa vitendo
vya ukatili katika jamii kwenye vyombo husika bila uoga. “Pale ambapo
mwanajamii anaona, anasikia au anahisi kuna ukiukwaji wa haki, ni wajibu wake
kuhakikisha suala hilo linaripotiwa mapema sehemu sahihi”.
Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa katika utekelezaji wa kampeni ya msaada
wa kisheria ya Mama Samia, wameamua kutumia falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo zimewezesha kwa kiasi kikubwa kuwa na misingi
imara ya utawala bora. “Hivyo ni jukumu la muhimu kwa Wizara ya Katiba na
Sheria kutekeleza falsafa hii kuhakikisha upatikanaji haki kwa wananchi katika
kujenga taifa lenye usawa, amani na maendeleo.”
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba,
Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Haroun
Ali Suleiman amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar, Kampeni hiyo imetoa msaada wa
kisheria kwa wananchi 422,908 ikiwa wanawake ni 209,185 na wanaume 213, 723
katika mikoa yote mitano ya Zanzibar jambo linaloashiria dhamira ya kweli ya
kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kupata haki.
“Kampeni hii imekuwa
hatua ya kihistoria katika kuhakikisha wananchi wote wanapata haki bila ya
kujali hali yao ya kiuchumi, kijamii au kijiografia.”
Kwa upande wake,
Naibu Kamishani wa Magereza Dkt. Justine Mhimba Kaziulaya amesema kuwa Jeshi la
Magereza kwa kushirikiana na Mashirika ya watoa Huduma za Msaada wa Kisheria
imefanikiwa kutoa huduma kwa wafungwa na mahabusu wapatao 15,664 nchi nzima
ambapo kati ya hao 2,998 walihudumiwa na 978 kati yao wameweza kupata dhamana
na kuachiliwa huru.
Kwa upande wake Rais
Chama cha Mawakili wa Serikali Bavoo Junusi amempongeza Rais Dkt. Samia kwa
kuasisi kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia baada ya kuona ipo haja ya
watanzania masikini na makundi maalum kupata huduma za kisheria bila malipo.
“Rais Dkt. Samia na
Serikali yake ni makini wasikivu na wanajali maslahi na ustawi wa watanzania,
sisi Mawakili tutahakikisha popote kampeni hii inapofika tunashiriki na kuunga
mkono ili watanzania wanufaike na kampeni hii.”
Naye, Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Usawa wa Jinsia
(UN Women), Bi. Hodan Addou ameipongeza Serikali kwa kuendesha kampeni ya
Msaada wa Kisheria kwa kuwa imesaidia kutoa haki kwa wasio na uwezo ikiwemo
wanawake pamoja na kukuza uelewa wa Sheria miongoni mwa Watanzania.” Tunafuraha
kuwa katika safari hii ya haki iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia.”



0 Maoni