Shirika la NHC lapata faida ya Bil. 235.4 miaka mitano

 

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limefanikiwa kupata faida ya Shilingi bilioni 235.4 katika kipindi cha miaka mitano (2018/19 hadi 2023/24), ikiwa ni ongezeko la faida kwa asilimia 33.1 katika kipindi hicho.

Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah Hamad, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea miradi mbalimbali ya shirika hilo ikiwemo Morocco Square, Kawe 711, Golden Premier Resident (GPR) na Samia Scheme Kawe.

Bw. Hamad amesema katika mwaka wa fedha wa Julai 2023 hadi Juni 2024, NHC imepata faida kabla ya kodi ya Shilingi bilioni 36.8, ikiwa ni sawa na asilimia 112.5 ya lengo, kwa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aidha, Bw. Hamad ameongeza kuwa mtaji wa Shirika umeendelea kuimarika, ambapo hadi kufikia Juni 2024 mtaji huo umefikia Shilingi trilioni 5.5, ukilinganishwa na Shilingi trilioni 5.08 mwaka uliopita.

“Katika kipindi cha miaka mitano (2019/20 hadi 2023/24), NHC imelipa kodi mbalimbali kwa Serikali zinazofikia jumla ya Shilingi bilioni 134.4, huku gawio kwa Serikali katika kipindi hicho kikifikia Shilingi bilioni 9.85,” alisema Bw. Hamad.

Kwa mwaka huu wa 2025 pekee, NHC imelipa gawio la Shilingi bilioni 5.5, na kufanikiwa kuweka rekodi ya kuwa shirika lililoongoza kwa ongezeko la gawio, hatua iliyowezesha kupatiwa tuzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Rais Dkt. Samia alitueleza kuwa anataka kuona NHC inatoa gawio la Shilingi bilioni 10, nasi tumejipanga kufikia huko na tuna timu nzuri yenye wataalam watakaoweza kufanikisha hilo,” aliongeza Bw. Hamad.

Kwa upande wa mapato, Mkurugenzi huyo alisema Shirika hilo limeendelea kuimarika, ambapo mapato yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 125 mwaka 2019/20 hadi Shilingi bilioni 189 mwaka 2023/24, sawa na ongezeko la asilimia 34.

Mapato hayo, kwa mujibu wa Bw. Hamad, tayari yamekaguliwa rasmi na CAG, jambo linaloonyesha uwazi na ufanisi wa uendeshaji wa shirika hilo la umma.



Chapisha Maoni

0 Maoni