Kesi ya kuchapisha
taarifa za uongo mtandaoni inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mhe. Tundu
Lissu imesikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu Jijini Dar es
Salaam, huku ikirusha live mtandaoni kesi hiyo kwa mara ya kwanza ili kutoa
fursa wa watu wengi zaidi kuifuatilia.
Tofauti na
ilivyofikiriwa kwamba pengine shauri hilo lingechukua muda mfupi kwakuwa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina nguvu ya kisheria ya kusikiliza shauri
hilo, badala yake imeshuhudiwa mvutano mkali wa kisheria baina ya mawakili wa
pande zote mbili.
Upande wa Jamhuri
kupitia Mawakili wake ilianza kwa kuieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri
hilo haujakamilika hivyo kuomba Mahakama kuhairisha kesi hadi siku nyingine, pia
Jamhuri iliibua jambo lingine kwamba
mtuhumiwa ameidharau Mahakama hiyo kwani wakati anaingia Mahakamani alitoa
manenoya 'No Reforms, No Election' jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Baada ya hoja hizo za
Jamhuri, Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mpale Mpoki, Dkt. Rugemeleza
Nshala, Peter Kibatala na wengineo walipinga vikali na kuiomba Mahakama kufuta
shauri hilo kwakuwa Jamhuri imeshindwa kukamilisha upelelezi kwa wakati, na
kwamba kitendo cha kuchelewesha upelelezi ni kumnyima mteja wao haki zake za
msingi ikizingatiwa kuwa kupitia shauri hilo mtuhumiwa hawezi kujibu chochote.
Kuhusu suala la mtuhumiwa
kutoa maneno wakati anaingia Mahakamani, Mawakili wake wameileza Mahakama kuwa
mtuhumiwa alicheleweshwa kuingizwa kwenye chumba cha Mahakama kwani ameingizwa
kwenye chumba hicho sambamba na wakati Hakimu wa kesi husika anaingia, jambo
ambalo limemkosesha mtuhumiwa uhuru wa kusalimiana na ndugu, jamaa na marafiki
zake waliofika kumuunga mkono
Akitoa maamuzi, baada
ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu anayesikiliza shauri hilo
amesema kwa mujibu wa sheria Mahakama inaanza tu pale Hakimu anapokuwa ameingia
kwenye chumba cha Mahakama na kwamba kiutaratibu mtuhumiwa anapaswa kuingizwa
kwenye chumba cha Mahakama baada ya Mahakama kuanza na si vinginevyo, hivyo
kutoa maelekezo kuwa utaratibu huo ndio unaopaswa kufuatwa hata itakapotajwa
kwa wakati mwingine.
Kuhusu suala la kutamka
maneno wakati Mahakama imeanza, Hakimu amekubaliana na hoja za Jamhuri kuwa ni
kweli mtuhumiwa Tundu Lissu ameidharau Mahakama kwa kitendo chake hicho cha
kutamka No Reforms, No Election.
Awali Mwenyekiti wa
Chadema Taifa, Tundu Lissu aliingia mahakamani na kauli mbili ya No Reforms, No
Election ndani ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Juni
2, 2025.
Mahakama imeihairisha
kesi hiyo hadi Juni 16, 2025, mtuhumiwa amerejeshwa rumande.
0 Maoni