WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim
Majaliwa ametoa wito kwa watafiti na wapangaji wa Sera kuwekeza katika tafiti
zenye tija kwa wananchi.
Amesema kufanya hivyo,
kutawezesha kuwa na matokeo ambayo yatatumika kutengeneza sera na mipango ya
utekelezaji yenye kuleta mabadiliko halisi katika jamii.
Mhe. Majaliwa ametoa wito huo leo Jumatano
(Juni 18, 2025) kwenye Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika chuoni hapo kampasi ya Mloganzila, jijini
Dar es Salaam.
“Tunataka kuona matokeo ya tafiti
hizi yanatumika, msiweke tafiti hizi kwenye makabati tu, matokeo haya yanapaswa
kuleta tija katika sekta ya afya, Ni matarajio yangu kuwa kongamano hili
litatumika kutoa mapendekezo
yatakayoimarisha mifumo, sera, na ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi
ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na mapinduzi haya”
Kadhalika, Mhe. Majaliwa
amewataka wadau wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika vifaa tiba, na
teknolojia mpya ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na magonjwa kwa wakati.
Amesema kuwa Serikali kwa upande
wake itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu,
rasilimali watu, tiba za kibingwa, na
mifumo ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa. “Tutaendelea kushirikiana na
wadau wote kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, salama na rafiki
bila kujali mahali alipo”.
Pia, Amesema kuwa Serikali ya
Awamu ya Sita inayoomgozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya
kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba ndani ya
nchi. “Tayari tumeanza kushuhudia hatua chanya katika maeneo haya, tukijivunia
mchango wa wataalamu wetu wa ndani”.
“Serikali yetu imeendelea
kuimarisha mazingira ya matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya. Leo hii,
hospitali zetu zinatumia mifumo ya kidijitali kubaini magonjwa, kutoa tiba
sahihi, na kufuatilia maendeleo ya wagonjwa.”
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu
Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu Prof. Daniel Mushi amesema kuwa
Serikali imeweka vipaumbele kwenye elimu, sayasi na teknolojia.
“Tunajivunia mageuzi
makubwa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, uongozi wake umeleta mageuzi
mapya katika kuimarisha taasisi za elimu nchini.”
Amesema kuwa maboresho yaliyopo
chuoni hapo ni ushahidi mkubwa wa namna serikali inavyoweka mipango ya
kuboresha mazingira ya Ujifunzaji na Kufundishia.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Appolinary
Kamuhabwa Ameipongeza Serikali kwa jitihada za dhati ambazo zimewezesha kuungwa
mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo na hivyo kufanikisha utekelezaji wa
miradi mikubwa ya kimkakati inayoleta mageuzi makubwa katika mazingira ya elimu
ya juu na afya nchini.
Prof. Appolinary amesema ujenzi
wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika
Mashariki (yaani "East African Centre of Excellence for Cardiovascular
Sciences") unaofadhiliwa na Serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika ni moja ya miradi itakayotekelezwa.
“Mradi huu unaingia katika awamu
ya pili, baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo hiki muhimu
hapa Mloganzila, Awamu ya kwanza iligharimu shilingi bilioni 21.62 na Awamu ya pili ya
mradi huu ambayo imeanza rasmi mwezi Mei 2025, inalenga kujenga Hospitali ya
Kisasa ya Kufundishia wataalamu bingwa na bobezi wa magonjwa ya Moyo na Mishipa
ya damu”. Alisema Prof. Appolinary.
Amesema kuwa Hospitali hiyo itakaongeza
uwezo wa kutoa huduma za
kibingwa, kufundisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi, na kufanya tafiti
zinazolenga kukabiliana na changamoto za magonjwa ya moyo na mishipa. “Awamu
hii itagharimu kiasi cha dola za shilingi bilioni 221.57.”



0 Maoni