MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya CCM anayoiongoza, imechukua hatua madhubuti katika kuweka mwelekeo wa elimu itakayotoa ujuzi na stadi za kazi kwa vijana ili kuwapatia sifa katika soko la ajira.
Rais Samia amesema
hayo leo Jumatano, tarehe 18 Juni 2025, wakati alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Amali ya
Sekondari Mwamapalala, Wilaya ya Itilima, kwa niaba ya shule zote 103 za
sekondari za amali zinazojengwa maeneo mbalimbali, nchini.
“Shule hizi na elimu
ya ufundi stadi tunalenga zitoe elimu ya ujuzi kwa vijana wetu ili wanapomaliza
wawe na sifa katika soko la ajira, kuajiriwa au kujiajiri. Shule hii tutaanza
masomo ifikapo mwezi Januari mwakani,” alisema Rais Samia.
Rais Dkt. Samia pia
aliwapongeza wananchi wa Itilima jinsi wilaya yao inavyopiga hatua za maendeleo
kwenye sekta mbalimbali, huku akiwasisitiza umuhimu wa kuwapatia watoto wao
fursa za kupata elimu, wakitumia ipasavyo miundombinu inayojengwa kwa gharama
kubwa na Serikali yao.
“Ndugu wananchi
wenzagu wa Itilima kwanza nawapongeza sana kwa hatua kubwa za maendeleo
mliyonayo. Leo nimeweka jiwe la msingi kwa niaba ya shule zingine zote za amali
zinazojengwa nchini. Nitakapozindua zikikamilika kujengwa, pia nitazindua kwa
niaba ya shule zote nchini.
Mhe. Rais Dkt. Samia
anaendelea na ziara yake yake ya kikazi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa
Simiyu, leo ikiwa ni siku ya nne tangu alipoanza siku ya Jumapili, tarehe 15
Juni 2025.


0 Maoni