Kwa mara ya kwanza
katika historia ya Tanzania, wanafunzi wa vijijini sasa wanasoma mubashara na
walimu walioko jijini Dar es Salaam kupitia ubunifu wa kiteknolojia ujulikanao
kama Darasa Janja.
Mradi huo ambao
umebuniwa na Mbunge wa Buchosa, Mheshimiwa Eric Shigongo, unalenga kutatua
changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi katika shule
za pembezoni hasa vijijini kwa kutumia teknolojia kama daraja la elimu.
Kwa kutumia vifaa vya
kisasa kama kamera za video, projecta, kompyuta na mifumo ya mawasiliano ya
intaneti, wanafunzi kutoka shule mbili tofauti sasa wanaunganishwa moja kwa
moja na mwalimu aliyepo jijini Dar es Salaam, wakifundishwa kwa wakati mmoja
kana kwamba wote wako katika darasa moja.
“Tuliamua kutotegemea
tena ahadi au wahisani. Maendeleo hayawezi kusubiri. Kama Mbunge, niliona kuna
njia ya kufanya jambo moja lifanyike sasa – kwa vitendo,” alisema Shigongo
katika mahojiano maalum.
Wanafunzi waliopata
fursa ya kushiriki katika Darasa Janja wameshuhudiwa wakiongeza ari ya
kujifunza, huku baadhi yao wakisema masomo ya Sayansi hayawatishi tena kama
zamani.
“Kwa mara ya kwanza
tunaona Sayansi ni kitu kinachowezekana. Tunaelewa zaidi kwa sababu tunamuona
mwalimu akielezea kwa vitendo,” alisema mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekondari
Nyehunge.
Walimu katika shule
husika pia wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema umewapa nguvu mpya ya
kushirikiana kwa karibu na wenzao walioko mjini huku wakijifunza mbinu mpya za
ufundishaji.
Mradi huu wa Darasa
Janja umetajwa na baadhi ya wadau wa elimu kama mfano wa namna ambavyo
teknolojia inaweza kutumika kufungua fursa kwa watoto wa Kitanzania bila kujali
walipo.
Katika jamii za
vijijini, mradi huu umeleta matumaini mapya. Wazazi, walimu na wanafunzi
wameshuhudia jinsi maono ya mtu mmoja, moyo wa kizalendo na uamuzi wa kufanya
jambo sahihi yanavyoweza kuleta mabadiliko ya kweli.

0 Maoni