JUMLA ya migodi 13,279 pamoja na bohari za baruti 164 zimekaguliwa nchini kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025.
Hayo yameelezwa leo
Mei 28, 2025 jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Idara ya Leseni wa Tume ya Madini,
Mhandisi Aziza Swedi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo,
Mhandisi Ramadhan Lwamo, katika kikao kazi cha wakaguzi wa migodi na baruti
kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesema kuwa miongoni
mwa migodi hiyo iliyokaguliwa ni migodi mikubwa saba, migodi ya kati 46, migodi
midogo 13,226 pamoja na bohari za baruti 164.
“Kaguzi hizi
zimeimarisha Sekta ya Madini na kuongeza makusanyo ya Serikali kupitia
maduhuli, hivyo kuchangia katika kuimarisha uchumi na Pato la Taifa,” amesema
Mhandisi Aziza.
Ameongeza kuwa,
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina
matarajio makubwa kwa Sekta ya Madini kutokana na mchango wake mkubwa katika
Pato la Taifa. Kufikia mwaka 2024, sekta hii ilichangia asilimia 10.1 ya Pato
la Taifa, ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 10 lililowekwa kufikiwa mwaka
2025.”
Mhandisi Aziza
ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa ya Idara ya Ukaguzi wa
Migodi, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha maduhuli ya Serikali katika sekta hiyo.
Aidha, amewakumbusha
wakaguzi kuzingatia Sheria ya Madini Na. 123 katika utekelezaji wa majukumu
yao, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu masuala ya
afya na usalama mahali pa kazi, uhifadhi wa mazingira, na matumizi salama ya
baruti ili kuepuka ajali.
“Naagiza kila mkoa
kutambua maeneo yenye hatari kubwa ya ajali na kuyawasilisha kwa Mkaguzi Mkuu
wa Migodi, ili kuweka mikakati shirikishi ya kuzuia ajali katika maeneo hayo,”
amesisitiza.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema
kikao hicho cha nne kwa wakaguzi wa migodi kinalenga kujengeana uwezo katika
utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuwa wao ni uti wa mgongo wa usimamizi wa
Sekta ya Madini.
“Wakaguzi wa migodi
wana jukumu kubwa. Malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yaliyowekwa na Serikali
hutegemea vyanzo vya mapato vinavyosimamiwa na wakaguzi. Bila kulinda vyanzo
hivyo, mapato hayawezi kupatikana. Tutaendelea kujifunza na kuboresha utendaji
ili kuhakikisha tunafikia malengo,” amesema Mhandisi Kamando.
Aidha, amebainisha
madhara ya kutofanya ukaguzi, yakiwemo ajali katika migodi zinazosababisha
vifo, kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji, na kupungua kwa
mapato ya Serikali.
0 Maoni