WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameendelea kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Japan
kuja kuwekeza kwenye sekta za kilimo, afya, uchumi wa buluu, nishati,
miundombinu, ufugaji na TEHAMA kwani Serikali imeshaboresha mazingira ya
ufanyaji biashara na uwekezaji.
Ameyasema hayo leo
(Jumatano, Mei 28, 2025) alipokutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa
Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu, Shirikisho la Wawekezaji
na Wafanyabiashara nchini Japan (KEIDANREN) na Jumuiya ya Wamiliki, Marais na
Watendaji Wakuu wa Mashirika na Makampuni wa Japan (KEIZA DOYUKAI).Waziri Mkuu
yuko Tokyo nchini Japan kwa ziara ya kikazi.
“Tunakaribisha makampuni ya Japan kuchangamkia
fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania, zikiungwa mkono na
mazingira tulivu ya biashara, mageuzi ya sera, na juhudi zinazoendelea za
kupunguza urasimu.”
Jana, Mei 27, 2025,
Mheshimiwa Majaliwa alikutana na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji
na Utalii wa Japan (MLIT), Kenichi Ogasawara pamoja na Rais wa Shirikisho la
Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu Japan na Afrika (JAIDA) Miyamoto Yaichi.
Katika mkutano huo
uliofanyika kwenye ofisi za MLIT na kuhudhuriwa na Marais wa makampuni makubwa
ya uwekezaji ya Japan, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji
hao nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za nishati, miundombinu,
utalii, kilimo na biashara.
Aidha, Waziri Mkuu
alisema kuwa Tanzania imejiimarisha katika kujenga uwezo wa rasilimali watu,
hivyo aliwakaribisha katika kutoa mafunzo na programu za kubadilishana maarifa
zitakazowezesha wahandisi wa Kitanzania, wapangaji miji, na wataalamu wa
miundombinu kunufaika na utaalamu na ubunifu mkubwa wa Japan.
Alisema Japan
imeendelea kuwa mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na kwa
kipindi cha miaka mingi, nchi hizo mbili zimejenga uhusiano thabiti, hasa
katika eneo la miundombinu. “Tunathamini sana uhusiano huu na mchango mkubwa wa
makampuni ya Kijapani katika maendeleo ya Taifa letu.”
Alisema Serikali
inaamini kuwa miundombinu bora ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi,
kuboresha maisha ya watu, kuwezesha biashara, na kuimarisha ushirikiano wa
kikanda. “Lengo la Tanzania kuendelea kuboresha mtandao wa barabara, reli,
bandari na viwanja vya ndege”.
“Haya ni maeneo
muhimu ya kuimarisha muunganiko wa ndani ya nchi na maeneo ya kikanda. Miradi
mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na upanuzi wa bandari za Dar es Salaam na
Mtwara ni mifano thabiti ya dhamira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha
usafirishaji wa kikanda.”
Kwa Upande wake,
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema kuwa
ametumia vikao kuwaeleza wawekezaji na wafanyabaishara hao kuhusu mipango na
mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inavutia zaidi uwekezaji katika sekta
mbalimbali.
Aidha, Mheshimiwa
Nyongo amesema kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuwa na dira ya Taifa ya
Maendeleo ya mwaka 2050 ambayo itaeleza kwa kiasi kikubwa itasaidia kubainisha
maeneo muhimu ya uwekezaji ili yanayolenga kukuza uchumi wa nchi.
Naye, Muwakilishi
Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNDP)
Shigeki Komatsubara amesema kuwa Tanzania itaendelea kunufaika na utaalam na
teknolojia kutoka Japan katika sekta mbalimbali zikiwemo za Miundombinu na
Rasilimali watu.
0 Maoni