Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema maendeleo ya
Tanzania katika uendelezaji miundombinu ni kutokana na ufanisi katika mapato ya
kikodi, ushiriki wa sekta binafsi pamoja
na uimarishaji wa masoko ya mitaji na dhamana inayotumika katika kufadhili
miradi hiyo.
Makamu wa Rais
amesema hayo wakati aliposhiriki majadiliano ya Viongozi wa Juu kuhusu “Umuhimu
wa kutumia Rasilimali za Bara la Afrika kwa ufanisi ili kuchochea Maendeleo”
yaliyofanyika wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Hoteli ya Sofitel Ivoire
Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
Amesema kutokana na
umuhimu wa miundombinu katika mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania, Serikali
ilihitaji kufanya kazi zaidi katika kukusanya fedha ya uendelezaji wa
miundombinu ikiwemo Reli ya kisasa (SGR) pamoja na barabara kuu ambazo
zitaunganisha mataifa mbalimbali na kuwezesha ufanyaji biashara.
Makamu wa Rais
ametaja juhudi za serikali katika ukusanyaji mapato ya ndani na kufadhili
miradi ikiwemo kuimarisha usimamizi wa kodi kama vile ukusanyaji kupitia mifumo
ya kielektoniki, kuwepo kwa Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya walipa kodi
ili kuwawezesha walipa kodi kuweza kutoa changamoto zao pamoja na kukuza wigo
wa soko la mitaji na dhamana kama vile uwepo wa hatifungani mbalimbali
Hatua zingine ambazo
Tanzania imepitia katika kuimarisha miundombinu ni pamoja na matumizi ya mifuko
ya hifadhi ya jamii katika ujenzi wa barabara na madaraja pamoja na kutumia
vema mikopo nafuu kutoka mashirika ya fedha kimataifa na nchi marafiki.
Makamu wa Rais
ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Rais wa AfDB
anayemaliza muda wake Dkt. Akinumwi Adesina kwa kushirikiana vema na Tanzania
katika kipindi cha uongozi wake ikiwemo kuwezesha ujenzi wa barabara, uwanja wa
ndege pamoja na reli ya kisasa (SGR) kuelekea nchini Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasia Kongo.
Makamu wa Rais
amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati kwa lengo la
kuharakisha maendeleo ikiwemo uwekezaji mkubwa katika mradi wa Bwawa la Mwalimu
Nyerere ambao umekamilika na unazalisha megawati 2115. Pia uwekezaji katika
miradi mingine ikiwemo matumizi ya gesi asilia pamoja kuanza uzalishaji wa
nishati ya joto ardhi ambayo itaanza kwa kuzalisha megawati 500.
0 Maoni