WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba Shigeru ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo
itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea
ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano
hayo.
Amekutana na kiongozi
huyo leo (Alhamisi, Mei 29, 2025) katika ofisi ya Waziri Mkuu Tokyo, Japan,
ambapo Mheshimiwa Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji
na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa
ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa pamoja na miradi mingine wanayotekeleza
nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya
Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya
Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha
nchini.
Amesema Waziri Mkuu
wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na
Balozi wa Japan nchini Tanzania Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo
na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali
ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya
Tanzania na Japan na kwamba ameahidi kuhakikisha makampuni mbalimbali ya Japan
yataendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi,
kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu
nchini inaendelea kuongezeka.
0 Maoni