TUME ya Madini imetoa leseni 8, 501 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025
ikilinganishwa na lengo la kutoa leseni 10,294.
Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma leo Mei 2, 2025 na
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde (MB) akiwasilisha makadirio ya mapato na
matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza Mhe. Mavunde amesema leseni za uchimbaji
zilizotolewa ni za uchimbaji mkubwa wa madini (SMLs) 1; leseni za uchimbaji wa
kati wa madini (MLs) - 25; leseni za utafutaji wa madini (PLs) 396; leseni za
uchimbaji mdogo (PMLs) ni 6,227.
Aidha, amesema leseni kubwa za biashara (DLs) zilizotolewa
ni 548; leseni ndogo za biashara (BLs)
1,290; leseni za uyeyushaji (RFLs) 1; na leseni za uchenjuaji wa madini
(PCLs) 13.
Waziri Mavunde amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi
Machi 2025, leseni 118 za utafutaji wa madini na leseni 41 za uchimbaji wa kati
wa madini zilipewa hati za makosa kutokana na kutozingatia masharti ya leseni
ikiwa ni pamoja na kutolipa ada za mwaka na kutoendeleza maeneo ya leseni.
Aidha, leseni tano za utafutaji madini na leseni tisa za
uchimbaji wa kati zilifutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa
hayo.
“Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili
ya wachimbaji wadogo ambapo hadi kufikia Machi 2025 maeneo 65 yametengwa katika
mikoa ya kimadini ikiwemo Geita, Mara, Mbogwe, Kahama, Chunya na
Songwe,”amesema Mhe. Mavunde.
Katika hatua nyingine, Waziri Mhe. Mavunde amesema sampuli
972 za makinikia ya Shaba zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi kutoka katika
migodi ya Bulyanhulu Gold Mine, Katavi Mining Company Limited, Jiuxing (TZ)
Mining Limited pamoja na ZEM (T) Company Limited.
Amesema, vilevile, sampuli 4,011 za wateja binafsi
zilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi lengo ni kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi
katika uchimbaji na biashara ya Madini.
Mhe. Mavunde amesema pia, kutokana na uchunguzi huo,
shilingi 296,732,000.00 zilikusanywa kama tozo stahiki za Serikali.
#MadiniBajeti
0 Maoni