WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema ushirikiano wa Tanzania na Japan umezidi kukua katika nyanja
za kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia umezidi kuimarika siku hadi siku, ambapo
mauzo ya biashara kati ya nchi hizo yameongezeka kutoka dola za Marekani
bilioni saba mwaka 2023 hadi bilioni 37 kwa mwaka 2024.
Mheshimiwa Majaliwa
ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 25, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho
ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan.
Amesema Wajapan
wanapenda sana bidhaa kutoka Tanzania zikiwemo za kilimo kama chai, kahawa,
ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo kama karafuu pamoja na
madini mbalimbali yanayopatikana nchini.
Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote
waje kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya elimu, afya,
miundombinu, nishati, kilimo, utalii kwani Tanzania imeweka mazingitra mazuri
ya uwekezaji na pia ina amani na utulivu.
“…Tanzania licha ya
kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na
mazingira tulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki,
Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba ambazo ni Uganda, Rwanda,
Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbuji hivyo
kuwawezesha wawekezaji kupata masoko ya uhakika katika mataifa hayo.”
Waziri Mkuu amesema
Serikali ipo katika mchakato wa kuvifanyia maboresho viwanja vya Maonesho vya
Mwalimu Julius Nyerere maarufu sabasaba ili viwe na hadhi ya kimataifa na
kuwezesha kufanyika mikutano na maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa.
Monesho hayo
yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanziba wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali.
Maonesho hayo
yalianza tangu Aprili 13, 2025 na yanatarajia kumalizika Oktoba 13, 2025, hii
ni mara ya pili kwa Japan (Osaka) kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ya kimataifa,
ambapo mara ya mwisho yalifanyika 1970 (EXPO 1970).
Kesho (Jumatatu, Mei
26, 2026), Mheshimiwa Majaliwa anatarajiwa kushiriki katika kongamano la
biashara, uwekezaji na utalii ambalo litahusisha wafanyabiashara kutoka
Tanzania na Japan. Pia, Waziri Mkuu atashiriki katika Mikutano ya Uwili na
viongozi wa Serikali ya Japan, mashirika ya maendeleo na watendaji wakuu wa
makampuni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya
Tanzania na Japan.




0 Maoni