Wawekezaji katika
Sekta ya Madini wamekaribishwa kuwekezwa katika mkoa wa Mtwara kutokana na
uwepo wa madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini mkakati yanayotumika kwenye
shughuli za viwanda.
Hayo yamesemwa
na Mhandisi wa Migodi Mwandamizi,
Michael Mtatiro alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa
huo, Winnifrida Mrema kupitia mahojiano maalum na wanahabari wanaoandaa kipindi
maalum cha kuangazia mafanikio katika Sekta ya Madini.
“Yapo madini mbalimbali yakiwemo yanayotokana na mchanga
wa bahari (Heavy mineral sands) yanayohusisha madini ya Rutile, Titanium,
Ilminite na Zircon” amesema Mtatiro.
Akielezea hali ya
makusanyo katika mkoa huo, Mhandisi Mtatiro amesema kuwa, Mkoa wa Mtwara
ulipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 9.18 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, na
kuongeza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 7.14 sawa na
asilimia 75 ya lengo lililopangwa.
“Tuna imani mpaka
mwisho wa mwezi wa sita tutakuwa tumefikia lengo la asilimia 100 la
makusanyo,” amesema.




0 Maoni