Wakati huku Afrika
tumezoea kuona watu wakigombania bidhaa mbalimbali muhimu za majumbani wakati
kunapotokea uhaba wake, wenzetu majuu hali ipo tofauti, ndio maana kuna baadhi
ya watu husema majuu kweli hamnazo. Hivi unaweza kuamini watu wazima wanaweza kugombani
midoli ?.
Hali ipo hivi mashabiki
wa midoli maarufu ya Labubu wameonyesha hasira zao mitandaoni baada ya
mtengenezaji wake kuondoa midoli hiyo kwenye maduka yote nchini Uingereza
kufuatia ripoti za wateja kupigania bidhaa hizo, ama kweli ukistaajabu ya Musa
utaona ya Firauni.
Kampuni
ya Pop Mart,
inayotengeneza midoli hiyo ya mnyororo wa begi yenye umbo la monsteri, iliambia
BBC kuwa imesitisha uuzaji wake katika maduka yake yote 16 hadi mwezi Juni ili
"kuepusha matatizo yoyote ya usalama yanayoweza kutokea".
Shabiki
wa Labubu, Victoria Calvert,
amesema alishuhudia vurugu katika duka la Stratford mjini London. "Ilikuwa ni hali ya kutisha kuwa katika
mazingira ambayo watu walikuwa wanapigana na kupiga kelele – na ilisababisha hofu."
Midoli
hiyo laini ilianza kuwa maarufu kwenye TikTok baada ya kuvaliwa na watu
mashuhuri kama Rihanna na
Dua Lipa. Sasa
baadhi ya wataalamu wa rejareja wanatoa tahadhari kuwa kusitishwa kwa bidhaa
hizo kutazidisha tu uhitaji.
Mdoli Labubu
ni kiumbe wa ajabu aliyechorwa na msanii wa Hong Kong, Kasing Lung, mzaliwa wa Hong
Kong, na alijulikana zaidi kupitia ushirikiano na duka la midoli la Pop Mart. Tangu walipopata umaarufu wa watu mashuhuri, midoli hiyo imekuwa
maarufu kama vifaa vya mitindo.
Nchini
Uingereza, bei zake huanzia £13.50 (Tsh 47,320) hadi
£50, (Tsh 182,000) huku matoleo adimu yakiuzwa kwa mamia ya
pauni kwenye tovuti za uuzaji tena kama Vinted
na eBay.



0 Maoni