Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Wanyamapori
ya Makuyuni inayojulikana kama "Makuyuni Wildlife Park” iliyopo Wilaya ya
Monduli, Mkoa wa Arusha waeleza ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika masuala ya uhifadhi na kijamii.
Wakizungumza katika nyakati tofauti Mei 24, 2025, wananchi hao wamesema kuwa viongozi wa Hifadhi ya Makuyuni wamekuwa wakiwapa ushirikiano wa kutosha katika masuala mbalimbali yakiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori na faida zitokanazo na shughuli za uhifadhi.
“Kiukweli ushirikiano kati ya wananchi na hifadhi upo, muda mwingine tunapokuwa tunapata changamoto hasa za kiusafiri, uongozi wa Makuyuni umekuwa ukitupatia usafiri ambao tunautumia katika operesheni ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu” amesema Justine Normas, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makuyuni Juu.
Sambamba na hilo, Normas ameongeza kuwa hifadhi ya Makuyuni imechangia katika ukuaji wa kipato kwa wananchi wa Kata ya Makuyuni kwa kutoa ajira za muda mfupi katika hifadhi.
“Ingawaje Hifadhi ni changa lakini kwa sasa tumeshaanza kuona matokeo na huko mbeleni tunatarajia kuona matokeo mengi zaidi, kiukweli tunaishukuru menejimenti ya Makuyuni kwani wanajitahidi kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya uhifadhi, na sisi kama viongozi wa kijiji tutaendelea kusisitiza wananchi kuhusiana na utunzaji wa mazingira ya hifadhi,” amesema Normas.
Kwa upande wake, Mmiliki wa kambi ya utalii inayojulikana kama Masai Eco Boma Lodge, Clamian Kitesho anashukuru kwa ushirikiano anaopewa na Hifadhi ya Makuyuni hususan katika utangazaji wa utamaduni wa jamii ya kimasai kwa kuzingatia kuwa kwa kupitia hifadhi hii idadi wa wageni wanaofanya utalii wa kiutamaduni katika boma lao umeongezeka.
"Kiukweli tunaushukuru uongozi wa Park kwa kutusemea vizuri kwa watalii wanaokuja kutembelea hifadhi, kwani watalii wanaokuja Park wengi wanakuja kulala kwenye boma zetu, na hii ni miongoni mwa faida tunayopata kwa hifadhi kuwa karibu na kijiji chetu," amesema Kitesho.
Pia, Kitesho ameongeza kuwa wao kama wananchi wa Kijiji cha Makuyuni wanafurahi Hifadhi hiyo kupewa jina la Kijiji chao kwani inafanya Kijiji cha Makuyuni kufahamika zaidi.
Naye, Emmanuel Meduke ambaye ni miongoni mwa vijana waliopata ajira ya kuongoza watalii katika Hifadhi ya Makuyuni amesema wao kama vijana wanafaidika na hifadhi hii kwa sababu wageni wakija wanakuja kwa ajili ya kutoa huduma.
“Kiukweli mimi ni miongoni mwa tunaofaidika na uwepo wa Park hii, pasipo hii hifadhi tusingekuwa tunapata hizi ajira tunazozipata saivi,” amesisitiza Meduke.



0 Maoni