Mkurugenzi wa Idara ya Afya Lishe na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amezielekeza timu ya usimamizi wa afya ya Mkoa wa Dar es Salaam (RHMT) na timu ya usimamizi wa afya (CHMT) katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuandaa mpango kazi wa kuwajengea uwezo wa matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika maeneo ya kutolea huduma za afya.
Dkt. Mfaume amesema hayo kwenye kikao cha majumuisho katika
hospitali ya Mbezi mara baada ziara yake yenye lengo la kuangalia upatikanaji
wa huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kwenye Halmashauri hiyo.
“Imefungwa mifumo mbalimbali ya TEHAMA katika vituo vyetu
vya kutolea huduma za afya lakini kufungwa tu haitoshi, tumeona kuna changamoto
kubwa sana ya uwezo wa watumishi wetu kutumia mifumo hii hivyo Halmashauri
iandae mpango kazi kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo,” amesema Dkt.Mfaume.
Amesema lazima
halmashauri ziwekeze kwenye TEHEMA kwa kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwa ni
muelekeo wa Dunia kwa sasa.
Aidha, Dkt. Mfaume amesema matumizi ya mifumo mbalimbali katika sekta ya afya yamekuwa na mchango mkubwa sana katika kuboresha huduma na kuongeza mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya.
0 Maoni