WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuwekeza
kwenye sekta ya madini ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata kipato na
kujikwamua kiuchumi.
Amesema Serikali
imenunua mitambo 15 ya kisasa ya uchenjuaji ambayo itasambazwa kwenye maeneo ya
wachimbaji wadogo hivyo ametoa wito kwa wachimbaji hao kujiunga katika vikundi
ili waweze kunufaika na fursa hiyo.
Ameyasema hayo leo
Jumapili (Mei 04,2025) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye kijiji cha Chingumbwa kitongoji cha Namungo Wilaya ya
Ruangwa Mkoani Lindi.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Afisa Madini
wa mkoa kuendelea na mpango wa kubaini maeneo yenye madini yatambulike na kisha
kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji.
“Pamoja na hili
tumeamua maeneo yote ya madini yaliyochukuliwa leseni na hayajaendelezwa kwa
muda mrefu, tutayachukua, tutayapima upya na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo.”
"Serikali yenu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia imenunua ndege maalum ambayo itasaidia kufanya tafiti ya kujua aina ya
madini yaliyopo na kiwango chake na sisi huku Lindi itakuja kuruka, Ruangwa na
maeneo ya Nachingwea”.
Akizungumzia sekta ya
barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na mipango ya
kuziboresha barabara mbalimbali katika wilaya ya Ruangwa ili kuziwezesha
kupitika wakati wote na hivyo kuwafanya wakazi wa maeneo hayo kufanya shughuli
mbalimbali za kiuchumi.
Naye Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Emmanuel Sengwaji
amesema kuwa Wataalam wa Idara ya Miradi mikubwa kutoka Tanesco wamefanya
uhakiki wa mahitaji ya umeme katika mkoa wa Lindi kutokana na ongezeko la
wawekezaji katika mkoa huo “Tuliomba tujengewe laini la gridi ya Taifa
itakayotoa umeme kutoka Masasi hadi Ruangwa katika eneo la Kitandi ili umeme
huo uweze kusambazwa maeneo ya uwekezaji ikiwemo kwenye migodi ya iliyopo
Kitongoji cha Namungo”.
Mheshimiwa Majaliwa pia alitembelea mgodi wa Elianje Genesis uliopo Namungo wilayani Ruangwa na kuona shughuli za uchenjuaji wa madini.
0 Maoni