Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed
Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kwa dhati
kuisogeza Serikali karibu zaidi na wananchi wake hasa wale walio na kipato cha
chini katika maeneo ya vijijini na mijini ili kuwaletea maendeleo.
Akizungumza kwenye Kongamano la Uchumi la Arusha jana Mei 3, 2025 jijini Arusha akiwa miongoni
mwa watoa mada, Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba lengo kuu ni kuwakomboa
wananchi kutoka katika mnyororo wa ukosefu wa taarifa, huduma na fursa, kwa kuwajengea
uelewa, uwezo na maarifa ya msingi, sambamba na kuwawekea miundombinu
inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mipango yao ya
maendeleo.
“Tupo katika zama ambazo maendeleo hayategemei tena maamuzi
ya viongozi wa kitaifa peke yao, bali yanategemea uwezo wa maeneo yetu ya mikoa
na halmashauri zetu kuongoza kwa dira, maarifa na maamuzi ya
kimkakati”.Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Aidha, amesema utawala bora siyo tu matumizi ya sheria bali
ni falsafa ya kuwezesha kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika ndoto ya
taifa na kujenga taasisi imara, kusimamia rasilimali kwa uadilifu, na kutoa
huduma kwa usawa bila upendeleo.
Amesisitiza kuwa kwa kutumia sera ya Decentralization by
Devolution (D-by-D), halmashauri zimewezeshwa kupanga na kutekeleza mipango yao
kulingana na vipaumbele vya wananchi wao na kwamba hiyo ndio njia ya kweli ya
kukuza demokrasia ya kiuchumi.
”Kwa maana hiyo, TAMISEMI imewapa halmashauri zetu nguvu ya
kufanya maamuzi kwa mujibu wa mazingira ya jamii zao. Hili linawezesha
uwekezaji wa ardhi, huduma bora kwa wananchi, na kuimarisha mapato ya ndani,”ameongeza
Waziri Mchengerwa.
Akifafanua zaidi amesema ustawi wa mikoa hautatokana na
maazimio ya makaratasi pekee, bali na uthubutu wa viongozi wake kuondoa
matabaka baina ya walionacho na wasio nacho ambapo amesisitiza mikoa ina wajibu
wa kufanya tafiti za kina za fursa zilizopo, kutambua changamoto kisekta,
kutafuta majawabu yanayotekelezeka na kuanzisha ubia mtambuka (multi-sectoral
partnerships) kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Waziri Mchengerwa ameagiza kwamba kongamano lisiwe tu mkutano wa mijadala, bali
chemchemi ya fikra mpya, dira ya uwekezaji wenye tija, na mlango wa fursa kwa
kila raia wa Mkoa wa Arusha iwe ni
kijijini au mijini.
Ametaka ongamano hilo
liwe chachu ya kufungua milango mipya ya uwekezaji kwa kushirikisha Wizara na
Taasisi zote husika za Serikali ili kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara
na uwekezaji yanaboreshwa kwa wepesi,
uwazi na ushawishi chanya.
Maeneo yaliyotambuliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa
ajili ya uwekezaji yaharakishwe kuhuishwa kwa kupangwa kitaalamu, kupimwa kwa
usahihi, fidia zote itolewe kwa haki, na miundombinu ya msingi (barabara, maji,
umeme, mawasiliano na huduma nyingine) ijengwe kwa haraka.
Amesisitiza kuwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali
washirikishwe kwa kina, kwa uwazi, na kwa heshima pasipo ubaguzi wa hali za kiuchumi, jinsia,
mila wala hadhi ya mtu.
Pia mchango wa wananchi wa kawaida unaojumuisha wakulima,
wafanyabiashara wadogo, vijana na wanawake lazima uwekwe kikamilifu kwenye
mpango unaotokana na Kongamano hili.
Aidha, ameelekeza sheria za nchi zisimamiwe kwa haki, weledi na uadilifu ili kulinda rasilimali za Mkoa na taifa na kwamba tusiruhusu migogoro isiyo ya lazima ififishe ndoto za mamilioni bali, tutumie maarifa ya ndani na teknolojia ya kisasa, kujifunza kutoka kwa uzoefu wa ndani na nje ya nchi, ili kubuni uwekezaji wa kisasa wenye tija na ustahimilivu wa muda mrefu.
0 Maoni