Serikali imesema vitambulisho vya Uandishi wa Habari (Press
Card), vitaanza kutolewa wakati wowote baada ya siku saba kuanzia jana Mei 3,
2025 baada ya Waandishi wa Habari kuanza kujisajili rasmi kwenye mfumo wa
TAI-Habari.
Mwandishi wa Habari ataanza kujisajili kupitia kiunganishi
cha https://taihabari.jab.go.tz kisha kufuata maelekezo yaliyotolewa ili
kukamilisha kujaza fomu yake kwenye mfumo huo wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi
wa Habari.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 03 Mei, 2025 na Katibu Mkuu wa
Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw.
Gerson Msigwa, katika Kijiji cha Sayu mkoani Shinyanga wakati akizungumza na
Waandishi wa Habari kuhusu masuala mbalimbali ya Miradi ya Maendeleo
inayotekelezwa na Serikali mkoani humo.
“Tuliwaahidi kwamba tunawaletea Press Card (Vitambulisho vya
kidijitali), ninayofuraha kuwajulisha kwamba 'press card' hizi za kidijital
mchakato umekamilika, ziko tayari kwa matumizi, siku saba kuanzia sasa mtaingia
kwenye kiunganishi cha Bodi ya lthibati ya Waandishi wa Habari na utaomba
kitambulisho...," alisema Bw. Gerson Msigwa.
Alisema Mwandishi wa Habari akishajaza taarifa zake sahihi,
Bodi itapokea maombi na kuyahakiki na kama yamekidhi vigezo kitambulisho
kitachapishwa na kutumwa mahali alipo kupitia Klabu za Waandishi wa Habari
katika maeneo yao.
“Ombi langu kwenu Waandishi wa Habari mtambue kitambulisho
hiki ni mali ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania…, hivyo
ukipewa wewe ndiye utakayewajibika kwa lolote litakalofanyika kwa utambulisho
wa kitambulisho hiki, siyo kitambulisho umekiacha huko, mtu amekichukua kaenda
kufanya utapeli tutambaini kwa sababu sasa tutakuwa tunaweza kufuatilia kwa
kupitia mfumo, tukibaini tutakupata wewe,” alisema Bw. Msigwa na kuongeza;
“Ninachowaomba kitunzeni kama mboni ya jicho, huu ndiyo
utambulisho wenu wa kazi, muwe nacho mfukoni, usikiache hovyo hovyo.”
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Wakili
Patrick Kipangula, ili kurahisisha zoezi la kutuma na kupokea Press Card hizo,
Waandishi wa Habari wanahimizwa kujisajili kwenye Klabu za Waandishi wa Habari
zilizopo maeneo yao.
Wakili Kipangula alisema wakati wa kujisajili Waandishi wa Habari wanapaswa kuweka kwenye mfumo vyeti vilivyo halali na kwamba ikiwa Mwandishi ataweka cheti cha kughushi, Bodi ya Ithibati itachukua hatua kali za kisheria kwa sababu hilo ni kosa la jinai.
Na. Mwandishi Wetu- JAB
0 Maoni