MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Chama cha Mapinduzi, Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa amesema kuwa Wilaya hiyo haina deni na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa ya kimaendeleo iliyofanyika katika sekta mbalimbali.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Mei 03, 2025) wakati
akizungumza katika kikao kilichojumuisha wajumbe wa Mabaraza ya Jumuia za Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Ruangwa kilichofanyika katika Bwalo Shule ya Awali
na Msingi ya Wonder Kids.
Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka
2010 hadi sasa ujenzi wa vituo vya afya umeongezeka kutoka vituo 2 hadi 12 hali
inayowezesha kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. “Tulikuwa na zahanati
22 lakini sasa zimefikia 35, na jitihada bado zinaendelea.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa
sekta ya elimu, Wilaya hiyo imewezesha kujenga shule za sekondari 30 kutoka
shule 16 za hapo awali.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa sasa Serikali
inatekeleza mradi mkubwa wa maji wa Nyangao - Ruangwa - Nachingwea ambao
unajumuisha vijiji 34 vya Wilaya ya Ruangwa, vijiji 21 vya Wilaya ya Nachingwea
na unatarajia kunufaisha wakazi 128,657.
Ameongeza kuwa Wilaya hiyo inaendelea na utekelezaji wa
ujenzi wa barabara za ndani ya wilaya pamoja na ujenzi wa mradi mkubwa wa
ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa ambao upo mbioni kukamilika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma
ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika
wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya ametaja baadhi ya miradi kuwa ujenzi wa
miundombinu ya barabara, vyumba vya madarasa, maji na vituo vya kutolea hiduma
za afya.
Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kuipa ushirikiano Serikali yao ambayo imejidhatiti kuendelea kuboresha huduma za kijamii.
0 Maoni