Tanzania yatoa uzoefu wa usimamizi endelevu wa misitu Tunisa

 

Wataalam kutoka Taasisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameungana na wenzao kutoka zaidi ya nchi 15 duniani katika mafunzo maalum ya siku tano kuhusu mbinu shirikishi za usimamizi endelevu wa ardhi na misitu, yaliyoandaliwa kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).

Mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Hammamet nchini Tunisia, yameangazia namna ya kuimarisha uhifadhi wa misitu kwa kutumia uasilia (nature-based solutions), sambamba na kuunganisha sekta muhimu za chakula, maji na nishati kwa ajili ya kujenga ustahimilivu wa ikolojia.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni nafasi ya misitu katika usalama wa chakula, upatikanaji wa maji safi, nishati mbadala na huduma za kiikolojia—na namna nchi zinavyoweza kuhuisha sera na mikakati ya pamoja katika maeneo hayo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka TFS, SACC Dkt. Zainabu Bungwa, aliwasilisha mada kuhusu uzoefu wa Tanzania katika usimamizi wa misitu kwa ajili ya kuhifadhi huduma za ikolojia, kuimarisha vyanzo vya maji, kukuza mnyororo wa thamani wa mazao mbadala kama vile ufugaji nyuki, na matumizi ya nishati endelevu vijijini.

Alieleza kuwa TFS kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiendesha miradi ya mfano ikiwemo Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF), ambapo misitu hutumika kama kiungo cha maendeleo ya jamii na mazingira.

Katika mafunzo hayo, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) nayo iliwakilishwa na Bi Caroline Sichwale, mtafiti mkuu wa masuala ya mbegu, ambaye aliwasilisha mchango wa tafiti za kitaifa katika kuimarisha uhifadhi wa ardhi kupitia kilimo endelevu.

Mafunzo hayo yalilenga kukuza uelewa wa pamoja kuhusu mbinu za SLM (Sustainable Land Management) na SFM (Sustainable Forest Management) kwa ajili ya kuunganisha kwa ufanisi sekta za maji, chakula, nishati na ikolojia.



Chapisha Maoni

0 Maoni