Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza upendo
na amani miongoni mwa Watanzania sambamba na kufanya jitihada mbalimbali
zitakazosaidia kuiletea nchi maendeleo.
Dkt. Biteko amesema
hayo leo Mei 25, 2025 jijini Mwanza aliposhiriki ibada ya maadhimisho ya Siku
ya Jumuiya ya Kikristu Tanzania - CCT Kitaifa iliyofanyika KKKT Ushirika wa Ebenezer - Pasiansi.
“ Niwahakikishie kuwa
milango ya Mhe. Rais Samia iko wazi,
anataka Tanzania moja ya watu wanaopendana na kushirikiana ili kuifikisha nchi mbele kimaendeleo,” amesema Dkt. Biteko
Ametaja jitihada za
Rais Samia kwa ajili ya kuleta amani, umoja na ushirikiano nchii kuwa ni pamoja
na mikutano yake ya viongozi wa dini, kuruhusu mikutano ya hadhara pamoja na
kuanzisha 4R’s yaani maridhiano, kuheshimiana, kujenga upya na kustahimiliana.
Kupitia ibada hiyo
Dkt. Biteko amewataka Watanzania kutogawanyika na kubaki wamoja sambamba na
kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na umoja na amani.
Amesisitiza kuwa ni
muhimu kwa Watanzania kuheshimiana na kustahiliana kwa kuwa watu wote hawawezi
kuwa na mawazo ya kufanana. Aidha, Serikali itamsikiliza kila mmoja ili kuwa na
Taifa lenye upendo na amani huku akiwaasa
wananchi kuheshimu sheria na katiba ya nchi.
Dkt. Biteko ameongeza
kuwa watu wakosoane kwa heshima na kupanda mbegu njema kwa wengine kwa kuwa kwa
mujibu wa vitabu vya imani kila analofanya mtu lina malipo yake. Huku
akisisitiza watu kutenda haki.
Katika hatua
nyingine, amesema Serikali, itaendelea kushirikiana na CCT na madhehebu yote
mengine ya dini kama ilivyowekwa msisitizo katika miongozo mbalimbali ya
Serikali ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996.
Ameongeza kuwa
Serikali inathamini mchango wa CCT katika jamii na maendeleo ya Taifa kwa
ujumla katika nyanja mbalimbali za afya, elimu, uchumi na malezi ya kiroho
pamoja na kudumisha amani nchini.
Amebainisha baadhi ya
maeneo ambayo yamefanyiwa kazi na CCT kuwa ni shughuli za umisheni na
uinjilisti ili kukuza uongozi wa kiroho miongoni mwa vijana na jamii kwa mfano
kupitia shughuli za UKWATA katika shule zote za sekondari nchini na USCF katika
vyuo vikuu na vyuo vya kati 92 nchini.
“ Mmetengeneza ajira kwa
vijana na jamii kwa mfano kutoka mwaka 2023 hadi 2025, mmetoa mafunzo ya walimu
200 wa sekondari na vyuo vya ufundi ili kuwasaidia wanafunzi katika ushauri wa
kitaaluma na stadi za maisha. Pia katika kipindi hicho hicho, mmewajengea uwezo
jumla ya vijana 45, 320 kuhusu masuala ya ajira na afya ya akili kupitia vyuo
mbalimbali nchini,” amesema Dkt. Biteko.
Kuhusu uchumi na
kilimo endelevu amesema kuanzia mwaka 2014 hadi 2025 wameanzisha na kusimamia
zaidi ya vikundi vya kiuchumi yaani VICOBA 1, 840 nchi nzima vyenye mtaji wa
zaidi ya shilingi bilioni 15 katika maeneo mbalimbali ikiwemo Bahi na Same.
Amezungumzia Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuhamasisha Watanzania kushiriki katika mikutano na
kugombea nafasi za uongozi.
Fauka ya hayo, Dkt.
Biteko ameipongeza CCT na kuitaka
kutoangalia tofauti za madhehebu yao bali kueneza injili nchini.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema kuwa mamlaka zinatoka kwa Mungu hivyo ametoa
wito kwa wananchi kuzitii mamlaka na wenye mamlaka wanatakiwa kutenda haki.
Pia, amewataka
wananchi Mkoa wake kuishi kwa upendo, kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii.
Awali, akihubiri
katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mt. Kilimanjaro
na Makamu Mwenyekiti wa CCT, Dkt. Stanley Hotay amesema kuwa haki ni kitu
ambacho mtu anastahili kuwa nacho na kuwa haki hizo zinalindwa na katiba ya
nchi.
Amesema wakristu
wanapaswa kujilinda kwa kuiombea nchi na mipaka yake hususan katika mikusanyiko
ya watu.
Katika kipindi cha
kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani amevishauri vyama
vya siasa kutumia maneno ya staha katika majukwaa yao na wala wasikubali
kushawishia kutenda uovu.
Kupitia ibada hiyo
iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania - KKKT,
Dkt. Alex Malasusa pamoja na maaskofu wa madhehebu ya kikristu 12 yanayounda
CCT, maaskofu hao waliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.
Na. Ofisi ya Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni