Mabalozi wa nchi tano
za Nordic ambazo ni Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden wameupongeza
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa mafanikio makubwa ya kuendeleza miradi ya upandaji miti na
uhifadhi wa mazingira, miradi ambayo iliasisiwa kwa msaada wa mataifa hayo
zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Pongezi hizo
zilitolewa jana, wakati wa ziara ya mabalozi hao mkoani Morogoro ikiwa ni
sehemu ya maadhimisho ya Nordic Week hapa nchini, ambapo walitembelea kituo cha
uzalishaji wa mbegu za miti kinachosimamiwa na TFS, kujionea shughuli
mbalimbali za uhifadhi wa misitu na uzalishaji wa miche.
Akizungumza kwa niaba
ya wenzake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, amesema
nchi zao zinafarijika kuona mchango wao wa miaka mingi ukizaa matunda katika
juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira nchini
Tanzania.
“Tumevutiwa na
jitihada mnazozifanya kupitia TFS. Miradi ya upandaji miti si tu kwamba
inasaidia kuhifadhi mazingira, bali pia inachochea maendeleo ya kiuchumi na
kijamii kwa jamii zinazozunguka misitu,” alisema Balozi Charlotta.
Kwa upande wake,Kamishna
msaidizi wa uhifadhi na meneja Baiolojiaya mbegu za miti TFS Fandey Mashimba
amesema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha usimamizi wa misitu ya asili na ile
inayopandwa, huku akiweka msisitizo kwenye uzalishaji wa miche bora na elimu
kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi.
“Nchi za Nordic
zimekuwa washirika wa muda mrefu katika sekta ya misitu. Mafanikio tunayoyaona
leo ni matokeo ya ushirikiano huo wa dhati,” amesema.
Naye Mkuu wa Kitengo
cha Uzalishaji Mbegu wa TFS, Mhifadhi Mkuu Mohamed Msalu, ameshukuru ujio wa
mabalozi hao, akisema ni ishara ya kuthamini kazi kubwa inayofanyika katika
kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira
na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
“Tunashukuru kwa ujio
huu wa mabalozi wa Nordic. Umetupa hamasa zaidi ya kuendeleza juhudi zetu za
kuhakikisha kuwa nchi inapata mbegu bora, zinazoweza kustahimili hali tofauti
za tabianchi na kuongeza misitu,” alisema Msalu.
Nordic Week ni wiki
maalum ya maadhimisho yanayolenga kuonesha utamaduni, ubunifu, biashara,
teknolojia na ushirikiano kutoka nchi za Nordic, huku lengo kuu likiwa ni
kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii na nchi mbalimbali,
ikiwemo Tanzania.
Kwa mujibu wa
mabalozi hao, mataifa yao yataendelea kushirikiana na Tanzania kupitia miradi
ya mazingira, elimu, nishati mbadala na masuala ya haki za binadamu kwa ajili
ya maendeleo endelevu.



0 Maoni