Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo
za Zege cha TCPM kutakidhi mahitaji ya Mkoa wa Tabora na maeneo mengine ya
jirani na kukuza uchumi wa nchi.
Kiwanda hicho kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha nguzo 120
kwa siku inadhihirisha kasi ya matumizi na uhitaji wa nguzo hizo za kisasa.
Pia, makadirio yanaonesha kuwa, mahitaji yanaongezeka na hivyo kuongeza fursa
kwa TCPM kulichangamkia soko hilo.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 3, 2025 mkoani Tabora
mara baada ya kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo za Zege cha TCPM.
“Niwapongeze uongozi wa Kampuni ya TCPM na wadau wengine kwa
jitihada zenu za kusimamia ujenzi wa Kiwanda hiki. Nimejulishwa kuwa
utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 73. Ni matumaini yangu kuwa,
asilimia iliyobaki mtaikamilisha kwa ufanisi na kwa kuzingatia muda na mahitaji
yaliyopo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameitaka TCPM kukamilisha mradi huo kwa kipindi cha miezi
miwili iliyobaki, sambamba na kulielekeza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuwapa TCPM shilingi bilioni 4 ili
kukamilisha mradi kwa haraka kwa kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ameelekeza wananchi wapate umeme.
Amesisitiza kuwa mahitaji ya umeme yanaongezeka kila mwaka
kwa asilimia 10 hadi 15 ukuaji ambao unadhihirisha umuhimu na uhitaji zaidi wa
miundombinu ya kisasa ikiwemo nguzo za
zege ambazo ni mbadala wa nguzo za miti.
Ameitaka TCPM kujenga nguzo bora ili kuwa mfano kwa kampuni
binafsi za kutengeneza nguzo.
Dkt. Biteko amebainisha manufaa ya Kiwanda hicho cha nguzo
za zege kuwa kitachangia ukuaji wa ajira za moja kwa moja na ajira ambazo
hutokana na mnyororo wa thamani.
Ametolea mfano “ Mwaka wa fedha uliopita 2023/2024
usambazaji ulikuwa nguzo 19,368. Lakini kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 hadi
kufikia mwezi Aprili usambazaji wa nguzo ulifikia 34,181. Sawa na ongezeko la
asilimia 76 ambayo hii tunaweza kusema ni ukuaji wa ajira ambayo itatengenezwa
na Sekta hii ya usambazaji wa nguzo za zege,”
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko ameeleza kuwa hadi sasa vijiji
vyote vimepata umeme na Serikali inaanza kupeleka umeme katika vitongoji nchi
nzima kwa kuanzia na vitongozi 20,000 huku Tabora ikipewa kipaumbele.
Aidha, Dkt. Biteko amehamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia na kusema kuwa Serikali inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya
Kupikia 2024- 2034 wenye lengo la kuhakikisha Watanzania asilimia 80 wanatumia
nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Dkt. Biteko amewataka
wananchi wa Tabora kutogawanyika kwa sababu yoyote ile huku akiwahimiza
kumuunga mkono Rais Samia kutokana na juhudi zake za kuwaletea wanachi
maendeleo.
" Katika uchaguzi Mkuu ujao tusikubali kugawanywa wala
kudanganywa kwa misingi yoyote ile, tukitanguliza tofauti zetu, matokeo yake
yataishi kwa kipindi kifupi na madhara yake yatakuwa ya muda mrefu"
amesema Dkt. Biteko
Naye, Mbunge wa Viti Maalum mkoani Tabora, Mhe. Munde
Tambwe amesema kuwa mkoa huo unazalisha tumbaku wa kiwango kikubwa hivyo wanaiomba
Serikali ijenge kiwanda cha tumbaku ili kutoa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felchesmi Mramba amesema tukio hilo ni muhimu ambalo litawezesha matumizi ya
nguzo ambazo ni imara na za gharama nafuu ikilinganishwa na nguzo za miti.
“Kuna baadhi ya maeneno nguzo za miti zimeshindwa
kustahimili mfano katika maji au dhidi ya moto lakini nguzo za zege zinadumu
muda mrefu na kuna baadhi ya maeneo mkoani Tanga ziliwekwa nguzo za zege na
zipo hadi leo pia zinatunza mazingira,” amesema Mhandisi Mramba.
Meneja Mkuu wa TCPM, Mhandisi Yusuph Kitivo amesema kuwa
Kiwanda hicho kinamilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania kwa
asilimia 100.
Amesema tayari nguzo hizo zimeanza kutumika katika mikoa ya
Katavi na Tabora na zaidi ya nguzo 80,000 zimeingia TANESCO na sasa kila wilaya
nchini ina nguzo za Kampuni hiyo ya zege zilizojengwa na wadau wao.
“ Mradi wa kujenga
kiwanda hiki ulianza rasmi mwaka Oktoba 30, 2024 ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za
kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika kwa kuwa na nguzo zinazodumu
kwa muda mrefu, umeme wa uhakika una chochea uchumi,” amesema Mhandisi Kitivo.
Amebainisha kuwa gharama ya mradi huo ni shilingi bilioni 6
na ujenzi utakamilika kwa viwango vinavyotarajiwa.
“ Kukamilika kwa kiwanda hiki kutasaidia ujenzi wa kiwanda kingine mkoani Mbeya na kutakuwa na manufaa makubwa kwa kuongeza pato la Taifa na kuzalisha ajira pamoja kukuza biashara mtambuka inayotokana na bidhaa hizi,” ameongeza Mhandisi Kitivo.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni