Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed
Mchengerwa ameweka jiwe la
msingi kwenye jengo la utawala la jiji
la Arusha na kushuhudia utiaji wa saini mikataba ya mradi wa Stendi Kuu ya Mkoa
wa Arusha, Soko la Mrombo na Bustani ya Mapumziko ya Themi vyote vikiwa thamani ya takriban shilingi bilioni 40.
Akikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya jiji
la Arusha lenye sakafu tisa ambalo litakapokamilika litagharimu bilioni 9.8 amemtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati ili
kuondokana na adha ya sasa ya watumishi kufanyia kazi kutokea kwenye ofisi zilizo katika maeneo
tofauti hali inayochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kutoa fedha za
ujenzi wa jengo hili kwa kuwa baada ya kukamilika litakuwa mkombozi kwa
watumishi," amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Aidha, ameuelekeza uongozi wa Mkoa na Jiji la Arusha
kuhakikisha jengo hilo linakamilika mara moja na endapo kutakuwa na mkwamo
wowote wachukue hatua.
Amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda kwa
kukwamua mgogoro wa kushindwa kukamilika kwa jengo hilo kwa zaidi ya miaka 5
kutokana na masuala ya kisiasa.
Mradi huo umefikia asilimia 62 na unafanywa na mkandarasi
mzawa M/S Tribe Construction Ltd na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.
Akihutubia wananchi baada ya kushuhudia utiaji wa saini
mikataba ya mradi wa ujenzi wa Stendi Kuu ya Mkoa wa Arusha na Soko la Mrombo
na Bustani ya Mapumziko ya Themi, Mhe. Mchengerwa amewataka viongozi kufanya
maaamuzi magumu katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa faida ya vizazi
vya sasa na baadaye.
Miradi hiyo ambayo inatarajia kugharimu bilioni 30.6
itakapokamilika ametaka iwe inaweza kujiendesha yenyewe na kutoa faida.
Pia amesisitiza kuilinda, na kufanya usafi ili iwezekudumu
kwa muda mrefu pindi itakapokamilika.
"Jukumu letu ni kuitunza miundombinu hii itakayojengwa
kwa gharama kubwa ili iweze kudumu kwa muda uliotarajiwa. Aidha, naelekeza
Halmashauri zenye Miradi yenye kujiendesha kama Masoko na Stendi zihakikishe
miradi hiyo inajiendesha na kuzalisha mapato kwenye Halmashauri husika," amesisitiza
Mhe. Waziri .
Amemtaka mkandarasi
kufanya kazi kwa haraka na kukamillisha kulingana na mkataba na mpango
kazi uliokubalika ili wananchi wa Jiji la Arusha waanze kunufaika na
miundombinu hiyo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika jijini
Arusha.
Aidha, amemtaka mkandarasi mshauri kuhakikisha mikataba hiyo
inasimamiwa kikamilifu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi na TARURA ili
ikamilike ndani ya muda uliopangwa, lakini pia katika ubora uliokubalika ili
thamani ya fedha ionekane.
Pia amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri wasimamie kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo kwa kutumia rasilimali watu na vifaa vilivyopo kwenye Halmashauri husika.
Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha maisha ya
Wananchi. Mojawapo ya hatua zinazochukuliwa ni kuboresha miundombinu ya usafiri
na usafirishaji, Masoko, pamoja utunzaji wa Mazingira katika maeneo ya mijini
chini ya Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji ya Tanzania kwa kuhusisha
Ushindani ambao kitaalam unajulikana kama Tanzania Cities Transforming
Infrastructure and Competitiveness (TACTIC) Project.
"Ndugu Wananchi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatekeleza kwa
vitendo falsafa ya maendeleo jumuishi. Miradi tunayoizindua leo kupitia Mradi
wa TACTIC siyo miundombinu pekee bali ni daraja kati ya leo na kesho bora zaidi
kwa wananchi wetu," amesisitiza.
Amesema miradi hiyo inatekelezwa kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia utakaogharimu kiasi cha Dola za Kimarekami Milioni 410 na inatekelezwa katika miji 45 mbalimbali nchini. Lengo kuu la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa Miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi.
0 Maoni