WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA)
limeihakikishia Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kuwa itaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.
Hatua hiyo imetokana
na namna ambavyo Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu matumizi ya fedha
mbalimbali zinazotolewa na wadau wa maendeleo likiwemo shirika hilo. Waziri
Mkuu amesema “Serikali itaendelea itaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote za
maendeleo zinazoletwa nchini na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.”
Ameyasema hayo juzi
(Jumatano, Mei 28, 2025) alipokutana na Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki
Katsura kwenye ukumbi wa Mikutano wa Tachibana uliopo katika hotel ya New
Otani, Tokyo nchini Japan akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Kadhalika, Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa JICA kuendelea kutafuta wadau zaidi wa
maendeleo kwa ajili upatikanaji wa fedha zitakazowezesha utekelezaji wa miradi
ya maendeleo na kuwafanya Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
Amesema lengo la wito
huo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa
malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa
wanafungua milango ya kiuchumi ili wananchi wengi washiriki katika miradi
mbalimbali ya maendeleo na kujiongezea kipato.
“Lengo la kutafuta
wadau hawa ni kuwawezesha wananchi washiriki kwenye shughuli mbalimbali za
kiuchumi, wanaotaka kuingia kwenye biashara, wanaotaka kuingia kwenye kilimo,
sekta ya madini, sekta ya uvuvi na ufugaji haya ni maeneo ambayo tumeyawekea
umuhimu.”
Waziri Mkuu amesema
Serikali inataka kuona wananchi wanaendesha shughuli za kibiashara kukiwa na
huduma zote katika mazingira rahisi, ikilinganishwa pia na utekelezaji wa
miradi ya elimu, afya, miundombinu, nishati, ujenzi wa barabara pamoja na
kilimo ni maeneo yanayotiliwa mkazo.
Kwa upande wake,
Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura alisema shirika lao linaendelea
kutekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo
Benki ya Dunia katika mradi wa Ustahimilivu wa Chakula.
Makamu huyo wa Rais
wa JICA alisema kuwa shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali katika
kufanikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ikiwemo ya kuimarisha sekta
ya miundombinu na usafirishaji.
Naye, Naibu Waziri wa
Kilimo, David Silinde ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa JICA kwa kushirikiana
na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mikopo yenye
masharti nafuu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 516 kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kilimo.
Mheshimiwa Silinde
ametaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Ustahimilivu wa Chakula (TSRP) unaogharimu
zaidi ya Dola za Marekani milioni 371 ambazo kati yake Benki ya Dunia imetoa
Dola milioni 300.05 na JICA imetoa Dola milioni 71.09, ambapo utekelezaji wa mradi
huo unafanyika kwa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.
Amesema mradi
mwingine ni wa Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP)
unaotekelezwa kwa ubia kati ya Benki ya Maendeleo Afrika na JICA unaohusika na
utoaji wa ruzuku katika pembejeo za kilimo.
Waziri Shilinde
amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 145, ambapo
kati ya fedha hizo, JICA wanatoa dola milioni 70 na AfDB dola milioni 75.49 na
ulianza kutekelezwa mwaka 2024 na utakamilika 2028. Tayari dola milioni 40
zimelipwa kwa kampuni 17 kwa ajili ya usambazaji wa mbolea.
Waziri Silinde
amesema fedha hizo zimetolewa baada ya wadau hao kuridhishwa na namna ambavyo
Serikali inasimamia sekta ya kilimo kwa mafanikio makubwa. Hata hivyo amewaomba
wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan waje kuwekeza katika kilimo cha
umwagiliaji hususan kwenye teknolojia ya umwagiliaji.
Naye, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Ali Mohamed Ameir amesema katika vikao hivyo
amewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan uwepo wa mazingira
wezeshi ya kutekeleza majukumu yao Zanzibar ikiwemo hali ya amani na utulivu.
Pia, Mheshimiwa Ameir
ametumia fursa hiyo kuiomba JICA kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
katika kukamilisha miradi miwili ya ujenzi ikiwemo upanuzi wa soko na jiko la
samaki katika eneo la Malindi hususani kutoa vifaa kwa wafanyabiashara pamoja
na mradi wa usambazaji maji mijini katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Miradi yote
inatekelezwa kwa awamu ya pili.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri
ameishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa kugharamia washauri elekezi
wawili ambao watakuwa kiungo kati ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na
Tanzania.
Amesema washauri hao
elekezi ambao watakuwepo TIC mmoja ni Mtanzania na mwingine Mjapani watakuwa na
majukumu ya kutoa taarifa za namna ya kufanikisha uwekezaji kati ya Tanzania na
Japan.
“Lengo la huyu
mwelekezi kutoka Japan ni kuzungumza na kusaidia makampuni na wawekezaji kutoka
Japan kupata taarifa za namna ya kuja kuwekeza Tanzania na huyu wa Tanzania ni
kusaidia Watanzania wote wanaotaka kuuza bidhaa zao Japan waweze kupata
usaidizi kupitia kituo cha uwekezaji.”
Awali, Meneja Uenezi
na Masoko wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema
ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka
2025) yanayoendelea nchini Japan umeiwezesha mamlaka yao kutangaza fursa za
uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.
Alisema mbali na
maonesho hayo, pia kitendo cha kushiriki katika mikutano iliyomhusisha Waziri
Mkuu pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Kijapan vilivyofanyika
jijini Tokyo alipata fursa ya kuelezea vipaumbe vya uwekezaji vilivyopo
Zanzibar ikiwemo uchumi wa buluu na utalii jambo ambalo liliwavutia wawekezaji
hao ambao tayari baadhi yao wameonesha nia ya kuwekeza Zanzibar.
0 Maoni