Wakati Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB)
ikiufungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa
https://taihabari.go.tz ili kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha
Uandishi wa Habari (Press Cards) Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg. Tido Mhando
amewaonya wenye nia ya kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa
zao.
Mhando alitoa tahadhali hiyo tarehe 19 Mei, 2025 wakati
akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari
katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam.
“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa
ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya
kidijiitali (digital Press Card). Maombi
ya ithibati Press Cards yatafanyika
kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari”, alisema.
Mhando alisema mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa
katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya
kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka
taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea
(Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati
shilingi Elfu Hamsini (50,000).
“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo
wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU
na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize
tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka
maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa
Sheria za nchi,” alisema Mhando.
Mhando alisema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha
mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha
huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha
upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.
Aliomba Wahariri, Waandishi na wadau wote wakiwemo waajiri
kutambua umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kuimarisha
weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na
hivyo watoe ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo
muhimu kwa taifa.
Akijibu maswali ya waandishi wa Habari kuhusu watu walio
kwenye tasnia bila kuwa na vyeti vya Elimu ya Uandishi wa Habari, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula alisema Sheria ilitoa
muda wa miaka mitano kwa watu waliokuwa hawana sifa ili wakasome na kutimiza
vigezo vya kisheria.
Alisema baada ya muda huo kuisha Waziri aliongeza muda wa
mwaka mmoja na kwamba tangu Waziri aongeze mwaka mmoja ni miaka miwili
imeshapita na kufanya jumla ya miaka nane na hivyo hakutakuwa na muda wa
nyongeza tena.
Na. Mwandishi Wetu- JAB
0 Maoni