TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wananchi kutoka
mikoa 16 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar wanaokwenda kuanza Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu yapili kujitokeza kuboresha taarifa zao
pamoja na kutazama daftari la awali la Wapiga Kura lililobandikwa katika vituo
walivyotumia kujiandikisha au kuboresha taarifa zao hap[o awali.
Hayo yamesemwa leo Mei 14, 2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele wakati akizungumza
na washiriki wa mafunzo ya siku moja ya watendaji wa Uboreshaji kutroka
Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoani Pwani.
“Niwasisitize watanzania wote katika mikoa hii 16,
wajitokeze kuja kuboresha taarifa zao au kuja kujiandikisha kwasababu baada ya
hapa Tume haita boresha tena Daftari…litaboreshwa kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei
kwa muda wa siku saba,”alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, mzunguko wa pili utahusisha mikoa ya Arusha, Manyara,
Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi,
Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na
Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.
Katika hatua nyingine Jaji Mwambegele amewakumbusha
watendaji hao wa uboreshaji ambao ni Waandikishaji Wasaidizi na waendesha vifaa
vya Biometriki kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za
Uchaguzi wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili ya zoezi hilo litakalofanyika
sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura.
“Nawakumbusha tena kama nilivyowakumbusha katika zoezi
lililopita, kwamba katika utekelezaji wa zoezi hili mzingatie sheria, kanuni na
taratibu za uchaguzi, muwe wanyenyekevu kwa wateja mtakao kuwa
mnawahudumia,”alisema Jaji Mwambegele.
“Zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu
cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka
2024 kinachoipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara
mbili mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa uchaguzi
mkuu unaofuata.
Nae Afisa Mwandikishaji wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha,
Dkt. Rogers Shemwelekwa amewataka wananchi wa Kibaha na viunga vyake kujitokeza
kutazama daftari la awali lililowekwa wazi na kama kuna changamoto waweze
kuziboresha wakati huu.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili
ulianza kufanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura
kuanzia tarehe 01 Mei, 2025 na kukamilika tarehe 04 Julai, 2025.
Uboreshaji wa Daftari unafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo
mzunguko wa kwanza ulihusisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikoa 16 na mzunguko
wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.
Mikoa iliyohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ni
pamoja na Iringa, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa,
Tabora, Katavi, Kigoma, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo
litafanyika kuanzia Mei 1 hadi 7 mwaka huu.
Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari
utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10
vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na
utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 04, 2025.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya
pili, utafanyika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania
Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vipo Tanzania
Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.
Katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya
1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na
wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea
kuwepo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.
Mambo mengine ni kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama
kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za
kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
Aidha, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2)
cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume
pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa
umma.
Lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa
wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa
pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa na
litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza.
Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 na kukamilisha tarehe 25 Machi, 2025.


0 Maoni