WAKAGUZI wa Migodi ya
Madini na Baruti wametakiwa kufanya kazi
kwa weledi, kuongeza ufanisi na
kufuata taratibu na sheria za nchi
katika utoaji wa huduma.
Hayo yamesemwa leo
Mei 29, 2025 na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi
Hamisi Kamando jijini Mwanza wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha
wakaguzi migodi na baruti ambacho kililenga kujengeana uwezo ikiwemo kufanya
maboresho ya Kanuni mbalimbali za madini
na Sheria ya Baruti.
‘’Tusikubali kuyumba
au kuyumbishwa na hatimaye kutolewa kwenye mstari, tuendelee kufuata misingi,
weledi na maadili katika utendaji kazi kwa kuepuka rushwa na kushinda
vishawishi na tamaa nyinginezo,’’amesema
Mhandisi Kamando na kuongeza,
“Nitoe rai,
tunatakiwa kuwajibika kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kuongeza bidii
kwenye kazi katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango
mkubwa kwenye Pato la Taifa."
Aidha, Mhandisi
Kamando amesema kuwa kikao hicho pia kimetoa mapendekezo ya maboresho ya Kanuni
za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira kwasababu zimepitwa na wakati kwa
kuwa maboresho ya Sheria za Madini Sura
ya 123 yalifanyika mwaka 2017 kwa mara ya kwanza na Kanuni husika
hazijarekebishwa hadi hivi sasa.
“Kutokana na
marekebisho ya Sheria ya Madini ni vyema
sasa tukafanya maboresho ya kanuni za usalama, afya na mazingira ili ziweze
kwenda sawa na Sheria na hivyo, kuimarisha ufanisi wa kazi, lakini pia kuna
Sheria ya baruti ya mwaka 1963 na kanuni zake za mwaka 1964 nazo tumeona
tufanyie maboresho ili usimamizi wa baruti nchini uwe mzuri zaidi,”amesema
Mhandisi Kamando.
Naye Mwanasheria
Mwandamizi wa Tume ya Madini, Damian Kaseko akiwasilisha mapendekezo ya Sheria
ya Baruti, Sura ya 45 ambayo ilitungwa mwaka 1963 ameeleza kuwa maboresho
yanayopendekezwa yanalenga kuboresha vifungu mbali mbali ili kuleta ufanisi
katika usimamizi wa utekelezaji wa sheria husika.
Kwa upande wake Siri
Boga, akizungumza kwa niaba ya washiriki amesema kikao kazi hicho kimewajengea uwezo wakaguzi wa madini huku wakipatiwa
mbinu mpya ambazo wanapaswa kuzifuata
wakati wa ukaguzi.
Wakati huo huo Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs), Maige Makolobela
akizungumza amesema kikao hicho ni muhimu kwa wakaguzi kupata mafunzo ya
pamoja, kubadilishana uzoefu na wenye migodi mikubwa.
“Tuna vijana
wameingia Tume ya Madini bado
hawajafahamu vitu vingi, hivyo ni fursa nzuri kwa vijana katika sekta yetu kujifunza kupitia
vikao kazi kama hivi,”amesema.
Amesema, sheria ya
baruti ni ya muda mrefu hivyo wamejaribu kuona
ni namna gani wanaweza kuiboresha
ukizingatia wakati inatungwa na hali ya sasa ni tofauti kutokana na
ongezeko la migodi.
0 Maoni