Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya
Sita aliyowasilisha ni ya mwisho katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020.
Amesema hayo Mei 29,
2025 wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM
Taifa - 2025 jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Ametaja maeneo sita
muhimu ya vipaumbele katika utekelezaji
wa Ilani hiyo ya CCM kuwa ni pamoja na kulinda
na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha
amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Dkt. Biteko
ameendelea kwa kusema kuwa eneo lingine ni kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na
shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na
miundombinu wezeshi.
Aidha, kipaumbele
kingine “ Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa
chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika
maendeleo ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu,
maji, umeme na makazi vijijini na mijini na kutengeneza ajira zisizopongua
milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana,” ameongeza Dkt. Biteko.
Katika hatua
nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa ikiwemo nchi
kuendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano pamoja na kuendelea kuenzi
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kudumisha Muungano wa Tanzania.
“ Vilevile, Serikali
imeendelea kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu kwa kuchukua
hatua mbalimbali ikiwemo kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa
na hivyo kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ili kuwezesha wananchi kupata
habari kwa wakati,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea
kusema kuwa mafanikio hayo yamechagizwa na falsafa aliyoianzisha Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 4R ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu,
Mabadiliko na Kujenga Upya.
Amesisitiza “
Falsafa hiyo imekuwa dira na nguzo
muhimu ya kisera katika kuijenga upya Tanzania yenye mshikamano, haki na
maendeleo endelevu kwa misingi ya demokrasia na ushirikishwaji wa wananchi
katika masuala ya msingi ya Taifa.”
Kupitia mkutano huo
Dkt. Biteko alielezea mafanikio ya Rais Samia kitaifa na kimataifa hususan
katika sekta ya nishati kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia barani
Afrika.
Akihutubia katika
mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mkutano Mkuu huo ni sehemu
muhimu ya maandalizi ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“ Kesho tutafanya uzinduzi wa Ilani tutakayoinadi kwa
wananchi ili kutupa nafasi nyingine ya kuongoza kwa miaka mitano,” amesema Dkt.
Samia.
Amebainisha kuwa Ilani hiyo imehusisha vipaumbele vya Chama na kuwa kabla ya kuiwasilisha kwa wajumbe wameona ni muhimu kupitia
utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020 hadi 2025.
Akizungumza katika
mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema lengo la
mkutano huo ni kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa
mwaka 2020 hadi 2025, kuzindua Ilani
mpya 2025 hadi 2030 na kupitia maboresho machache ya Katiba ya CCM.
Aidha, Mkutano huo
ulioongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan umehudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa nchini, mabalozi
wanaowakilisha nchi zao Tanzania pamoja wawakilishi wa vyama rafiki kutoka nchi
mbalimbali za Afrika, China na Korea ya Kaskazini na Urusi.
0 Maoni