Balozi wa Tanzania
katika Ufalme wa Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi, tarehe 29 Mei, 2025, alifanya
kikao na Watanzania wanaoishi nchini humo katika viwanja vya ofisi za ubalozi
jijini Stockhom.
Katika kikao hicho
kilicholenga kufahamiana na kujadiliana kuhusu masuala ya Diaspora, Mhe. Balozi
Matinyi alielezea tafsiri ya neno "diaspora" kwa mujibu wa Sera ya
Mambo ya Nje ya mwaka 2001, toleo la mwaka 2024, iliyozinduliwa tarehe 19 Mei,
2025, jijini Dar es Salaam na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Balozi
alieleza kuwa sera hii inawatambua Diaspora kuwa ni raia wa Tanzania wanaoishi
nje (Citizen Diaspora) na raia wa nchi zingine wenye asili ya Tanzania
(Non-Citizen Diaspora).
Mhe. Balozi Matinyi
aliwaeleza Watanzania hao waliotoka miji mbalimbali ya Uswidi, kwamba sera hiyo
imetambua ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya nchi yetu huku akirejea wito
wa Mhe. Rais Dkt. Samia wa kuwataka Diaspora wawekeze nchini ili kuchangia
maendeleo ya taifa.
Akiinukuu hotuba ya
bajeti bungeni ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, Mhe. Balozi Matinyi aliwaambia kwamba kwa
mwaka 2024 Diaspora wa Tanzania waliwekeza fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.5
katika mfuko wa UTT-AMIS na shilingi bilioni 9.28 kwenye sekta ya milki kupitia
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na sekta binafsi.
Baada ya mazungumzo
hayo Mhe. Balozi Matinyi aliwataka wajenge umoja na ushirikiano kama alama kuu
za Watanzania popote walipo duniani na kupigania maslahi ya nchi
yao wakati wote.
0 Maoni