WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amempongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo imeshuhudiwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umetokana na umarishaji wa ukusanyaji wa mapato
nchini. “Bila shaka, kila mwananchi ni shahidi wa jambo hili. Hakika Mheshimiwa
Rais anastahili pongezi na tunampongeza sana.”
“Ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya kuiongoza nchi yetu kwa
mafanikio makubwa. Sote ni mashahidi kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya
uongozi wake, Ilani ya Uchaguzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa.”
Mheshimiwa Majaliwa
ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 15, 2025) wakati akiwasilisha hotuba yake
ya kuhitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa
Bunge kwa mwaka 2025/2026 aliyoiwasilisha Bungeni Jumatano, Aprili 9, 2025.
Amesema sambamba na
kudumisha hali ya amani, utulivu pamoja na mshikamano wa wananchi, Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo
pamoja na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
“Mathalan, katika kipindi cha mwezi Julai hadi
Machi, mwaka wa fedha 2024/2025, Mamlaka ya Mapato Tanzania imekusanya kiasi
cha shilingi trilioni 24.05 sawa na ufanisi wa asilimia 103.62 ya lengo.”
Aidha, makusanyo hayo ni ya
kiwango cha juu kabisa kufikiwa na TRA kwa kipindi kama hicho tangu kuanzishwa
kwake. “Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 77 ikilinganishwa na kiasi
cha shilingi trilioni 13.59 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa
fedha 2020/2021.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema
ufanisi uliofikiwa katika makusanyo ni matokeo chanya ya kutekeleza kwa vitendo
maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha
mazingira ya ulipaji kodi.
“…Serikali inawapongeza
walipakodi nchini kutimiza wajibu wao kwa kulipa kodi stahiki kwa wakati na
kuendelea kuunga mkono kizalendo juhudi za Serikali za kuleta maendeleo nchini
kwani “Kodi Yetu Ndiyo Maendeleo Yetu.”
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa mchango
wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa. Vilevile, awapongeza waajiri, viongozi wa
Vyama vya Wafanyakazi na wadau wote kwa kuendelea kuheshimu haki na
utu wa wafanyakazi.
0 Maoni