TAARIFA KWA UMMA
KUH; KUKEMEA NA KUCHUKUA HATUA DHIDI YA MABINTI WANAFUNZI WA
VYUO VIKUU WALIOMDHALILISHA BINTI MWENZAO.
Dar es Salaam, 20 Aprili, 2025.
Ndugu Wananchi, Pamoja na Heri ya Pasaka kwenu wote,
nasikitika kuwapa taarifa kuwa, usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka tarehe 20
Aprili, 2024 nilipokea tags nyingi kupitia mtandao wa Instagram wakinitumia
video kadhaa zinazoonesha mabinti kadhaa wakishirikiana kumdhalilisha binti
mwingine kwa maneno na vipigo na mambo mengine mabaya ambapo, watoa taarifa
walidai kuwa, mabinti hao wote ni wanafunzi wa vyuo vikuu viwili tofauti nchini
huku wengine wakidaiwa kuwa, wanasoma darasa moja na huyo binti
wanayemdhalilisha na kumrekodi. Aidha, kwenye mazungumzo yao kama
yanavyosikika, inaonekana ni ugomvi wa kumgombania mwanaume anayetajwa kwa jina
moja la Mwijaku.
Binafsi, nimesikitishwa sana kusikia mabinti wasomi ambao,
wangetakiwa kujikita kwenye elimu na kuunganisha nguvu kupambana kutokomeza
ukatili dhidi ya wanawake na watoto badala yake wanatumia nguvu zao na elimu
zao kukatiliana, kudhalilishana na kujidhalilisha wao kwa wao. Udhalilishaji
waliofanya kwa Binti mwenzao haukubaliki kabisa na unastahili kukemewa kwa
nguvu zote, kwani ni kinyume na sheria zote na pia siyo utu wala siyo haiba ya
mwanamke wa Dunia ya sasa kwamba, akipishana jambo na mwanamke mwenzie au mtu
yeyote, basi amfanyie udhalilishaji kwani, huko ni kujidhalilisha yeye mwenyewe
na kudhalilisha wanawake wote.
HATUA NILIZOCHUKUA:
1. Nimewasiliana na manusura na kumuunganisha na huduma za
ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia na huduma za Dawati la Jinsia Polisi
ambapo, pia atapata Msaada wa kisheria ili haki itendeke.
2. Nawasiliana na Wakuu wa Vyuo husika kupitia Madawati ya
Jinsia kwenye Vyuo husika Ili hatua za nidhamu zichukuliwe kupitia Sheria na Miongozo
ya Vyuo husika dhidi ya waliofanya udhalilishaji huu.
3. Nawasiliana na Waziri mwenye Dhamana na Elimu, Sayansi na
Teknolojia pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa hatua zaidi.
WITO KWA WANANCHI KWA UJUMLA IKIWEMO WANAFUNZI WA NGAZI MBALIMBALI: tuache kumaliza migogoro kupitia utaratibu wa kudhalilisha wengine.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum - Dk. Dorothy Gwajima.

0 Maoni