BALOZI wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi,
amesema kuwa atatumia uzoefu alioupata katika kazi yake ya uandishi wa habari
kutafuta taarifa na kung'amua mbinu za kuvutia watalii wengi kama ilivyo katika
nchi hiyo ambayo inavutiwa na kutembelewa na watalii wengi.
"Nitakapofika katika nchi hizo tisa katika eneo langu
la uwakilishi nitahakikisha ninatafuta na kujua ni mbinu gani wanazotumia
kuvutia watalii kwani watalii wengi duniani huenda kwenye nchi hizo," alisema
Mhe. Balozi Matinyi.
Alisema pia kuwa kwa kutumia uzoefu wake katika uandishi wa
habari - fani ambayo hujenga tabia ya udadisi na mbinu za kutafuta taarifa za
uwekezaji na pia tabia kulikamilisha jukumu la kazi baada ya kulichukua.
Balozi Matinyi alisema hayo hivi karibuni katika mahojinao
maalumu na kituo cha televisheni cha ZBC cha Zanzibar.
Alifafanua kwa kueleza kuwa diplomasia ya uchumi nchini
ilianzishwa katika utawala wa awamu ya tatu ambapo ili kuujenga uchumi wetu
baada ya kumaliza kuzisaidia nchi zingine za Afrika kupata uhuru.
"Hii ndiyo sababu viongozi wetu wakuu wanatusisitizia
kwamba tunapokwenda nje ya nchi tukaifanyie kazi diplomasia ya uchumi,"
alidokeza Mhe. Balozi Matinyi.
"Nitakapofika katika nchi hizo tisa zilizoendelea
kiuchumi, katika sekta ya uvuvi, kilimo katika viwanda vya mbolea na matrekta,
utalii ambapo wanapokea watalii kati ya milioni 6 hadi 7 kwa mwaka wakitumia
visiwa vingi na bahari kuvutia watalii, jukumu langu litakuwa kuhakikisha
tunapata mbinu zao na Watanzania tunasonga mbele kiuchumi," alisema Mhe.
Balozi Matinyi.
Aidha, akizungumzia namna atakakavyoiwakilisha Zanzibar,
alisema kuwa tayari ameshapata maelezo mbalimbali kutoka taasisi za uwekezaji,
kama za uchumi wa buluu na utalii na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kujua
namna ya kuielezea Zanzibar.
"Tuna nchi tisa katika eneo ninalokwenda wenye tabia ya
kutaka kufahamu vyakula vya watu wengine; hivyo, nitawaeleza kwamba Zanzibar
kuna viungo vya kipekee vyenye ladha nzuri."
Mhe. Balozi Matinyi
amezitaja nchi ambazo atakuwa mwakilishi mbali ya Sweden kuwa Denmark, Finland,
Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukrane.
Akijibu swali kuhusu mgogoro wa nchi za Ukraine na Russia,
Mhe. Balozi Matinyi alisema kuwa Tanzania inasimamia amani na hivyo inataka
nchi zinapokwaruzana zitafute suluhu kwa mazungumzo na si kupigana vita.
0 Maoni