Wananchi wa Kijiji cha Nditi, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, wameanza kuona manufaa ya vituo vya Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wakisema kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo.
Wakizungumza Aprili 13, 2025
katika mkutano wa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na wanyamapori hao,
wananchi hao walieleza kuwa uwepo wa kituo cha kudumu cha askari katika eneo
hilo umeleta utulivu na kuwawezesha kurejea katika shughuli za kilimo bila
hofu.
"Kabla ya kituo hiki
hatukuwa na amani, lakini sasa tembo wakionekana tunapata msaada kwa haraka.
TAWA wametujengea kituo hapa Nditi, tunawashukuru sana," alisema Saidi
Juma Ngomo, mkazi wa kijiji hicho.
Ameongeza kuwa kwa miaka
minne iliyopita, wakulima walikuwa wakikumbwa na hofu kubwa mashambani, lakini
sasa hali imebadilika kwa kiasi kikubwa na jamii imeanza kuelewa umuhimu wa
kuwa karibu na askari wa wanyamapori.
Wananchi hao wameiomba
Serikali kuongeza idadi ya askari na vituo kama hivyo katika maeneo mengine ya
wilaya ili kuhakikisha mapambano dhidi ya wanyamapori waharibifu yanakuwa
endelevu na yenye tija zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Mohamed Moyo, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha mifumo ya
ulinzi dhidi ya wanyamapori wakali.
"Kupitia baraza la
madiwani tumepitisha bajeti ya kununua ndege nyuki kwa ajili ya kuimarisha
jitihada za kudhibiti tembo. Hii ni dhamira ya kweli ya kuwalinda wananchi wetu
na mali zao," alisema Mhe. Moyo.
Akizungumza katika mkutano
huo, Afisa Uhifadhi Mkuu wa TAWA kutoka Kanda ya Kusini Mashariki, Linus Chuwa,
alisema kuwa Mamlaka hiyo imejenga vituo vitano vya kudumu katika maeneo yenye
changamoto ya migogoro baina ya binadamu na tembo.
Alivitaja vituo hivyo kuwa
ni pamoja na kile cha Kijiji cha Ngarambe (Rufiji), Milola (Lindi Manispaa),
Nditi (Nachingwea), Chingurunguru (Tunduru), na Ngumbu (Liwale). Kila kituo
kikiwa na askari waliopatiwa vifaa maalum vya kazi kama mabomu ya baridi na
silaha za kisasa kwa ajili ya kutawanya wanyama bila kuwatisha wananchi.
Naye Afisa Habari wa TAWA,
Beatus Maganja, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wananchi
wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi kwa kuhakikisha wanapata msaada wa haraka
pindi wanapokumbwa na changamoto ya wanyamapori.
"Serikali haitakaa
kimya kuona wananchi wake wakiteseka kwa sababu ya tembo. Tumejipanga
kuhakikisha usalama wa watu na mali zao unalindwa kwa nguvu zote,"
alisema Maganja.
0 Maoni