Shule ya Sekondari ya
Mwambisi Forest iliyopo Kibaha, mkoani Pwani, imeibuka mshindi wa kwanza
kitaifa katika kampeni ya upandaji miti iliyoandaliwa na Benki ya NMB, na
kuzawadiwa Shilingi milioni 50.
Akizungumza wakati wa hafla
ya kukabidhi zawadi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye alikuwa mgeni
rasmi, aliipongeza Benki ya NMB kwa kuandaa kampeni hiyo, akisema imekuwa
kichocheo muhimu kwa jamii katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na upandaji
miti.
Waziri Mchengerwa aliwataka
wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala kote nchini
kuhakikisha kila halmashauri inatekeleza agizo la Makamu wa Rais la kupanda
miti milioni 1.5 kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu
wa Fedha wa Benki ya NMB, Ndg. Juma Kimori, alisema benki hiyo imetambua kwa
vitendo umuhimu wa mazingira na iliahidi kupanda miti milioni 1, lakini imevuka
lengo hilo kwa kupanda miti milioni 1.4.
Akizungumza kwa niaba ya
Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu nchini, Prof. Dos Santos Silayo, Naibu Kamishna
wa Uhifadhi wa Misitu kutoka TFS, Bw. Hamza Katete, alisema mahitaji ya bidhaa
kutoka kwenye rasilimali za misitu nchini ni zaidi ya mita za ujazo milioni
62.3 kwa mwaka, huku uwezo wa misitu iliyopo kuzalisha ukiwa ni mita za ujazo
milioni 42.8 pekee, hali inayoonesha pengo kubwa linalopaswa kuzibwa kupitia
juhudi za upandaji miti.
Mbali na Shule ya Mwambisi
Forest kuibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia Sh milioni 50, Shule ya Msingi
Ibondo kutoka Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza ilishika nafasi ya pili na
kuzawadiwa Sh milioni 30, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Shule ya
Sekondari Itimba ya Wilaya ya Mafinga, mkoani Iringa ambayo
ilizawadiwa Sh milioni 20.
0 Maoni