Mkuu wa
Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, Bw. Zakaria Mwansasu, amesema kwamba
kiwanda cha kuchakata mafuta ya parachichi cha Avoafrica kimekua mkumbozi wa
wakulima wa parachichi wa mkoa huo na mikoa jirani.
Bw. Mwansasu ameyasema
hayo jana wakati wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania walipotembelea
kiwanda hicho wakiwa nji njiani kurejea Dar es Salaam kutoka Ruvuma, kwa
mwaliko wa Mkuu wa Mkoa Njombe Mhe. Anthony Mtaka.
Amesema
kwamba zamani wakulima walikuwa wanakosa mahali pa kuuzia parachichi ambazo
hazijakidhi vigezo vya kuuzwa nje ya nchi na kujikuta wakipata hasara kutokana
na kukosa wateja ama kuuza kwa bei ya chini mno.
Amesema
kwamba tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha Avoafrica sasa mambo yamebadilika
kwani wakulima wamepata soko la uhakika la parachichi ambazo hazikidhi mahitaji
ya soko la nje ya nchi na matokeo yake kuchochea kasi ya ukuaji wa kilimo cha
zao hilo.
Kwa upande
wake Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda hicho Megan Kabuje akiongea kwa niaba ya
meneja wa kiwanda hicho amesema kwa sasa wananunua parachichi hizo kwa bei ya
shilingi 700 kwa kilo na bei itaendelea kuongezeka kadri ya muda unavyokwenda.
“Hapo awali
wakulima wa parachichi walikuwa wakipata hasara kwa kukosa soko na hata
waliobahatika kuuza walikuwa wakiuza kwa shilingi 100 kwa kilo, lakini sasa
wamepata soko la uhakika kwa kuuza shilingi 700 kwa kilo,” alisema Bw. Kabuje.
0 Maoni