Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amesema, jukumu la kuiokoa Jamii na ukatili
wa kijiinsia ni la kila mmoja hivyo ameiasa Jamii kushirikiana katika kupambana
na vitendo hivyo.
Dkt. Jingu ameyasema hayo jana jijini Dodoma wakati
akiongoza kikao cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili
dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024.
Dkt. Jingu ameeleza kuwa, licha ya mafanikio yanayoendelea
kushuhudiwa kama vile kuimarika kwa huduma kwa waathirika wa ukatili na
kuongezeka kwa uelewa wa jamii, bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji
kushughulikiwa kwa haraka na umakini.
"Changamoto kama umasikini wa kaya, ndoa na mimba za
utotoni, ukatili wa kingono na kisaikolojia bado ni tatizo kubwa. Tunahitaji
ushirikiano wa kweli baina ya sekta zote ili kuhakikisha MTAKUWWA inatekelezwa
kikamilifu," amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
wa maendeleo, asasi za kiraia na Taasisi nyingine kuhakikisha lengo la
kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 linafikiwa.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Nandera Mhando,
amewataka washiriki kwenda kusimamia vizuri majukumu yao ikiwa ni pamoja na
kuzingatia maelekezo na majumuisho ya kikao hicho ili kutekeleza na kufikia
malengo ya MTAKUWWA ya kutokomeza ukatili, kwani utekelezaji thabiti wa mpango
huu unahitaji dhamira ya dhati, uwajibikaji na usimamizi makini kutoka kwa kila
mdau katika ngazi zote kuanzia Serikali Kuu hadi mitaani.
Aidha washiriki wa kikao hicho wamepongeza uongozi wa Wizara kwa mwelekeo mzuri katika kuratibu MTAKUWWA pamoja na uwasilishaji wa taarifa na majadiliano yenye tija, huku wakiahidi kwenda kutekeleza maelekezo yote kwa bidii, uwazi na ushirikiano ili kuhakikisha jitihada za kutokomeza ukatili zinazaa matunda katika jamii.
Na. WMJJWM - Dodoma
0 Maoni