Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mh. Emily Burns leo wamekutana Jijini Dodoma na kufanya kikao juu ya maendeleo ya sekta ya madini nchini.
Balozi Emily Burns ambaye pia ametumia kikao hicho kwa ajili
ya kujitambulisha, amesema nchi ya Canada ipo tayari kushirikiana na Tanzania
katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini kwa kuwajengeza uwezo katika
uchimbaji wa matumizi sahihi ya Teknolojia utakaozingatia utunzaji wa mazingira
na kuwajengea ujuzi ili kuongeza tija kwenye uzalishaji madini.
Aidha Balozi Burns ameonesha utayari wa serikali ya Canada
kutoa mafunzo maalum (Tailor-made training) kwa wakinamama na Vijana kupitia
vyuo vya Ufundi-VETA katika maeneo ambapo uzalishaji madini unafanyika kwa
wingi.
Balozi Burns ametumia pia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa
Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa mageuzi makubwa yanayofanyika kwenye sekta ya
madini hadi kupelekea kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la
Taifa kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024.
Waziri Anthony Mavunde ameishukuru serikali ya Canada kwa
dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta ya madini huku
msisitizo mkubwa akiuweka katika ushirikiano wa Utafiti wa Kina wa upatikanaji wa madini nchini ili kusaidia
upatikanaji wa taarifa sahihi za uwingi wa madini nchini.
Waziri Mavunde pia ameonesha umuhimu wa uwezeshaji wa Wakina mama na Vijana kupitia Programu ya Mining for a brighter Tomorrow (MBT) yenye lengo la kuyawezesha makundi hayo mawili katika ushiriki wake katika uchumi kupitia sekta ya madini.
0 Maoni