Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Jijini Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi kwa njia ya mtandao Aprili 28, 2025 kuhusu hoja za pingamizi za mawakili wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Kesi hiyo imesikilizwa leo kwa njia ya mtandao mbele ya
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini ambapo upande wa Jamhuri kupitia wakili
Nassoro Katuga, umesema kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya Lissu kusomewa
maelezo ya awali, katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni huku
kesi ya uhaini ikiwa ni kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo Lissu na Mawakili wake, wanapinga utaratibu wa
kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao huku wakitaka mtuhumiwa afikishwe
mahakamani ili asomewe Maelezo ya Awali kwani ni lazima upande wa Jamhuri,
utetezi na mtuhumiwa wawepo mahakamani, pamoja na mshtakiwa kusaini karatasi ya
maelezo.
Katika kesi hiyo, Lissu anatetewa na jopo la mawakili 31
wakiongozwa na wakili Mpale Mpoki ambaye aliungana na Alute Mugwai, Peter
Kibatala na Jeremiah Ntobesya kuwasilisha mapingamizi.
Wakili Mpoki amedai kuwa hata kama mtuhumiwa angekuwepo mtandaoni leo, wasingeweza kuendelea kwa sababu ingekuwa ni kinyume cha sheria kwa sababu sheria inataka maelezo ya awali yafanyike mtuhumiwa akiwepo.
0 Maoni