Serikali kupitia Wizara ya Madini imetunga kanuni za msaada
wa kiufundi katika Leseni ndogo za uchimbaji wa Madini ambapo zitaratibu
ushiriki wa wageni katika Leseni ndogo za uchimbaji wa Madini(PML) ambazo kwa
mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Madini sura ya 123,kimezitamka Leseni
hizi kama maalum kwa ajili ya Watanzania.
Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini kinatoa ruhusa kwa
mmiliki wa Leseni ndogo ya uchimbaji madini kuingia ubia na mgeni kwa
makubaliano ya msaada wa kiufundi (𝙏𝙚𝙘𝙝𝙣𝙞𝙘𝙖𝙡
𝙎𝙪𝙥p𝙤𝙧𝙩).
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka
2024/25 Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde alisema Serikali inatarajia
kutunga kanuni za kuratibu ushiriki wa wageni katika Leseni ndogo kwa kuwa
kumejitokea wimbi kubwa la wageni kuingia katika maeneo ya wachimbaji wadogo
kwa mgongo wa “Msaada wa Kiufundi” ambao haukuwa na utaratibu mzuri na hivyo
kupelekea wachimbaji wengi wadogo kutopata manufaa yaliyokusudiwa ya
kujiimarisha kupitia Leseni ndogo za uchimbaji na wakati mwingine katika
vikundi vya wachimbaji viongozi wachache kuingia makubaliano ya msaada wa
kiufundi bila kushirikisha wahusika wote na hivyo kuzua migogoro isiyo na
sababu.
Tarehe 25.04.2025 limetolewa Tangazo la Serikali Na. 260
kuitambulisha kanuni hii mpya kuanza utekelezaji wake ikiwa ni ahadi
iliyotolewa na Waziri Mavunde akitekeleza maelekezo ya Mh. Rais Dkt. Samia S.
Hassan.
Kanuni hiyo imetaja mambo mengi muhimu, yakiwemo;
1. Usajili wa Mikataba ya Kiufundi kwenye Tume ya Madini
baina ya Mchimbaji Mdogo na Mtoa Msaada wa kiufundi.
2. Kufafanua maana ya maneno “Msaada wa Kiufundi” ili kutimiza lengo
mahsusi la kuongeza tija ya uzalishaji na kukuza ujuzi.
3. Mgawanyo wa Mapato kati ya Mwenye Leseni Ndogo na Mtoa msaada wa Kiufundi kwa madini yatakayozalishwa.
0 Maoni