Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/2026 ya kiasi cha shilingi Trilioni 2.2 ambapo asilimia 96.5 ya Bajeti yote ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na asilimia 3.5 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.
Akiwasilisha Bajeti hiyo tarehe 28 Aprili, 2025 bungeni
jijini Dodoma, Dkt.Biteko ametaja vipaumbele mbalimbali vya Wizara ya Nishati
kwa mwaka 2025/2026 ikiwemo kuendelea kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji wa umeme, pamoja na kufikisha Gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia
ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara.
“ Mhe. Spika, kipaumbele kingine ni kuendelea na usambazaji
wa nishati katika vitongoji, maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji
pamoja na vituo vya afya ili kuwezesha shughuli za uzalishaji na utoaji wa
huduma bora kwa wananchi,” ameeleza Dkt.Biteko.
Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni upatikanaji wa umeme wa
uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha
Gridi ya Taifa na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha
umeme.
Pia kuhamasisha na kuwezesha watanzania kutumia nishati safi
ya kupikia ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi
ya Kupikia (2024-2034) na Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 – 2030.
Dkt. Biteko ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa umeme
wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha
Gridi ya Taifa na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha
umeme.
Pia, kuendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta
vijijini kupitia ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa kipaumbele kingine cha Bajeti ya
2025/2026 ni kutekeleza shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa
mafuta na gesi asilia na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta
na gesi asilia.
Vilevile kusimamia na kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa
upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja kuimarisha matumizi ya gesi
asilia (CNG) katika vyombo vya moto.
Ameongeza kuwa kipaumbele kingine ni kuendelea kutekeleza
shughuli za kiudhibiti kwa kuimarisha
ushiriki wa wazawa katika Sekta ya Nishati pamoja na kuimarisha nguvu kazi na
kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi ili kuimarisha tija na ufanisi katika
utendaji kazi.
Pia kuongeza mchango
wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na ushiriki wa Sekta Binafsi
katika maendeleo ya Sekta ya Nishati na kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa
wa Nishati wa Mwaka 2025 - 2030 (National Energy Compact 2025 - 2030) kuhusu
upatikanaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi.
Awali Dkt.Biteko alilieleza Bunge la Tanzania kuhusu
mafanikio mbalimbali ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha
2024/2025 ikiwemo kukamilika kwa mradi wa kielelezo wa kuzalisha umeme kwa
Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) – MW 2,115 na ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 160 kutoka
kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere hadi Chalinze mkoani Pwani.
Ametaja mafanikio
mengine kuwa ni kukamilika kwa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza
umeme cha Chalinze na kuingiza umeme unaozalishwa JNHPP kwenye Gridi ya Taifa
pamoja na kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400
kutoka Singida hadi Arusha.
Mafanikio mengine yaliyopatikana katika Bajeti ya 2024/2025
ni kuongezeka kwa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyounganishwa katika
Gridi ya Taifa kutoka MW 1,601.84 Mwaka 2020/21 hadi MW 4,031.71 na kukamilika
kwa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze na kuingiza umeme
unaozalishwa JNHPP kwenye Gridi ya Taifa.
Pia kukamilika kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya
msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na kuunganisha Mkoa wa
Kigoma kwenye Gridi ya Taifa na kufanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni
58.4 zilizokuwa zinatumika kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya dizeli
katika mkoa wa Kigoma.
Katika usambazaji wa umeme vijijini, Dkt. Biteko amesema
kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imefikisha miradi ya umeme
katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kutoka vijiji 506 vilivyokuwa
vimeunganishiwa umeme mwaka 2007 wakati REA inaanzishwa. Pia, kufikisha umeme
kwenye vitongoji 33,657 kati ya 64,359 sawa na asilimia 52.
Dkt. Biteko ametaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilika kwa
ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa
kilomita 115 kutoka Tabora hadi Urambo na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme Urambo pamoja na kuongezeka kwa uhamasishaji na matumizi ya
nishati safi ya kupikia ikiwemo usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia
266,000 na majiko banifu 5,000 kwa wananchi.
Mafanikio mengine ya Bajeti ya 2024/2025 ni kuimarika kwa
upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na kufungwa kwa
mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa MW 20 katika eneo la
Hiyari – Mtwara pamoja na kuongezeka kwa wateja waliounganishiwa umeme nchini kutoka 2,766,745 Mwaka 2020/21
hadi 5,449,278 mwezi Aprili, 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 97.
Katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia, Dkt. Biteko amesema kuwa
kumekuwa na ongezeko la mtandao wa usambazaji wa gesi asilia nchini kutoka
kilomita 102.54 Mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 mwezi Aprili 2025 ambao
umewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57.
Vilevile kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa TPDC katika
Kitalu cha uzalishaji wa gesi asilia cha Mnazi Bay kutoka asilimia 20 hadi
asilimia 40 na kutolewa Leseni ya Uendelezaji wa Kitalu cha kuzalisha gesi
asilia cha Ntorya kwa TPDC ambayo itashirikiana na Kampuni ya ARA Petroleum katika uendelezaji
wa kitalu hicho.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa vituo vya kujaza gesi
asilia (CNG filling stations) kwenye vyombo vya moto kutoka vituo viwili (2)
Mwaka 2020/21 hadi vituo tisa (9) mwezi Aprili 2025 pamoja na kuongezeka kwa
ushiriki wa Watanzania katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi
asilia hadi asilimia 90 ikilinganishwa na mwaka 202.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo ameeleza kuwa katika Bajeti ya mwaka
2024/2025, Wizara ya Nishati imetekeleza vipaumbele vyake kwa kiwango cha
kuridhisha ambapo Kamati hiyo imepongeza Viongozi Wakuu wa Wizara ya Nishati
pamoja na Watendaji kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa Kamati hiyo lengo
likiwa ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Nishati inakuwa na mafanikio.
Kuhusu Bajeti ya Mwaka 2025/2026 Kamati imeishauri Wizara ya
Nishati masuala mbali ikiwemo kuzidi kufuatilia upatikanaji wa fedha za
utekelezaji wa miradi ya nishati, malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha
miradi,TANESCO kuongeza kasi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme pamoja na kuendeleza
miradi ikiwemo ya kusafirisha umeme ili wananchi wapate umeme wa
uhakika.
0 Maoni