Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewaasa wakristo kuliombea Taifa amani, utulivu, umoja na mshikamano
uendelee ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 20, 2025 jijini Mwanza
wakati aliposhiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la African Inland Church
(AIC) - Makongoro.
“ Mwaka huu ni wa uchaguzi na una michakato mbalimbali ya
kujiandikisha, kugombea, kupiga kura na kutangaza matokeo. Kwa niaba ya
Serikali napenda kuwaomba waumini wa AICT na wale ambao tunadhani tuna uwezo wa
kugombea nafasi mbalimbali tujitokeze kwa wingi tugombee, wale tu wenye nia ya
kweli tuhakikishe tunawasaidia watu katika hali zao,” amesema Dkt. Biteko.
Sambamba na kugombea amewahimiza waumini kuliombea Taifa
kuelekea wakati na baada ya uchaguzi “ Tujitokeze ili tuweze kugombea kwa ajili
ya kuhudumia nchi yetu na wakati wa kampeni utakapofika naomba tuendelee
kuliombea Taifa.”
Ameongeza kuwa Mwl. Julius Nyerere na viongozi wengine
waliweka misingi imara ya amani na kushikamana wakati wote na Tanzania
inafahamika duniani kote kama kisiwa cha amani hivyo waumini hao waliombee
Taifa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya katika Taifa na kuendelea kufanya
nchi kuwa na amani.
Amebainisha “Tuliyofundishwa kwenye ibada ya leo ni pamoja
na kuwa ilikuwa kusudi la Mungu kwa Yesu afufuke na tunamshukuru Mungu kwa
ajili ya siku ya leo ya kutufanya kuwa hai na sisi waumini wa Kanisa hili kukutana
hapa na kuabudu kwa pamoja.”
Pamoja na hayo Dkt. Biteko amewaeleza waumini wa Kanisa hilo
kuwa kufufuka kwa Yesu ni ishara ya ushindi na kuwa wote wameshinda pamoja na
Yesu kama alivyoshinda mauti, watashinda pia katika kukamilisha ujenzi wa
Kanisa lao ambalo wanaendelea kulijenga.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania
(AICT) Musa Masanja Magwesela amesema waumini hao watumie nafasi ya kufufuka
kwa Yesu kwa kuleta mabadiliko katika maisha yao.
Awali akihubiri katika ibada hiyo, Mchungaji wa Kanisa la
African Inland Church kutoka Turkana nchini Kenya, Stephen Kilel amesema kuwa
tukio la Yesu kufufuka ni tukio kuu linalowapa ujasiri wa kujua imani yao ni
thabiti.
“ Wapo watu wengine
ambao hawaamini kama Yesu amefufuka. Sisi tunaweza kupata matumaini makubwa
kumbe maisha yetu hayaishi pale ambapo kifo cha mwili kimetupata, kuna ufufuo
ambao unatupa nguvu ya kuzungumza juu ya habari njema,” amesema
Mchungaji Kilel.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati



0 Maoni