Benki ya Dunia imeipongeza
Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ujenzi wa shule mpya
zilizojengwa kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari SEQUIP ambao
umepunguza umbali kwa wanafunzi kufuata elimu suala ambalo lilikuwa
likiwakatisha masomo yao hasa jinsia ya kike.
Pongezi hizo zimetolewa na
Huma Kidwai Mtaalamu wa Elimu kutoka Benki ya Dunia ambaye ni Mtaratibu wa
Mradi wa SEQUIP kwa niaba ya Benki ya Dunia baada ya kutembelea shule ya
Sekondari ya Amali ya Katerero iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba ambayo
imejengwa kupitia mradi huo katika Mkoa wa Kagera.
Akisistiza umahiri wa
wanafunzi katika shule hizo mpya, Kidwai amewashauri Wakuu wa shule hizo
kujifunza mbinu mpya kwa shule Kongwe na kuwa wabunifu ili kuzalisha wanafunzi
bora na mahiri.
Akizungumza kwa niaba ya
Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mratibu wa Mradi wa SEQUIP Richard Makota amesema
shule hizo zilizojengwa zinalenga kuwasaidia wanafunzi kupata elimu kwa vitendo
na nadharia kutokana na miundombinu iliyowekwa hasa kwa masomo ya Sayansi.
Aidha, Ferdinand Eladius
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Amali ya Katerero akizungumza kwa niaba ya walimu
wenzake amesema uwepo wa shule hiyo umewasaidia wanafunzi kupenda masomo kutokana
na upekee wa miundombinu iliyopo.
Na. OR – TAMISEMI - Kagera
0 Maoni