Mheshimiwa Macocha M.
Tembele, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia ameshiriki katika Mdahalo maalum
kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 70 ya Mkutano wa Afrika na Indonesia maarufu
kama Mkutano wa Bandung.
Mdahalo huo uliofanyika jana
umeandaliwa na Kituo cha Mikakati na Masomo ya Kimataifa (Center for Strategic
and International Studies- CSIS) cha Indonesia na kuongozwa na kaulimbiu
isemayo The Global South in a Shifting World Order: Challenges, Aspirations,
and the Road Ahead.
Aidha, mdahalo huo
umehudhuriwa na Mheshimiwa Arif Havas Oegroseno, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
wa Indonesia pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo mabalozi, wahadhili wa vyuo
vikuu, wanafunzi n.k.
Kwa upande wake Mheshimiwa
Balozi Tembele pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa, Tanzania ni miongoni
mwa nchi za mwanzo kabisa zilizoshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa
misingi ya ushirikiano, mshikamano, usawa na ukombozi zilizoasisiwa katika
Mkutano wa Bandung wa mwaka 1955 kupitia ushiriki wake katika uanzishwaji wa
Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), pamoja na harakati za
ukombozi wa nchi za Afrika.
Vilevile, Mheshimiwa Balozi
alizungumzia kuhusu umuhimu wa mataifa ya Ulimwengu wa Kusini kudumisha fikra
za Bandung kwa kuimarisha zaidi ushirikiano kiuchumi kupitia Taasisi na Jumuiya
zake za Kikanda kama vile Umoja wa Afrika (AU) na ASEAN.
Halikadhalika, Mheshimiwa
Balozi alitoa wito kwa nchi za Ulimwengu wa Kusini kuangalia uwezekano wa
kuzifanyia mapitio agenda za Bandung ili ziweze kuakisi hali ya sasa ya kidunia
na kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani kwa kujumuisha maeneo
mapya ya ushirikiano kama vile mabadiliko ya tabianchi n.k.
0 Maoni