Waziri wa Maji Mh. Jumaa
Aweso amewataka wataalamu wa Wizara ya Maji kuhakikisha wanaongeza nguvu ya
utafiti wa kina wa maji katika Jiji la Dodoma ili kusaidia upatikanaji wa maji
safi na salama kwa wananchi wa Jiji la Dodoma.
Waziri Aweso ameyasema hayo jana
wakati akikagua miradi ya maji wa Nala unaogharimu Tsh 3.8 bn na Uchimbaji wa
Visima katika kata ya Nkuhungu na maeneo mengine ya Jiji mradi wenye thamani ya
Tsh 41bn.
“Ni maelekezo ya Mh Rais
Dkt. Samia S . Hassan kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji Jijini Dodoma na
ndio maana zimetolewa fedha zaidi ya Tsh 45bn kupelekea upatikanaji wa maji.
Ninaelekeza wataalamu wa
wizara kuhakikisha unafanyika utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji Dodoma
Jiji kwa kuchimba visima virefu maeneo mbalimbali.
Ninaelekeza mitambo ya
uchimbaji visima iongezwe hapa Dodoma na ile Timu ya wataalamu waliokuwa kwenye
usimamizi wa mradi wa Same Mwanga sasa kuhamia Dodoma mpaka tuhakikishe
tunaongeza vyanzo vya kutosha vya maji,” alisema Aweso.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma
Mjini Mh. Anthony Mavunde ameshukuru hatua ambazo zinachukuliwa na serikali
kukabiliana na upungufu wa maji na kusema miradi hii miwili ikikamilika
itaongeza uzalishaji maji kufikia lita 121m kw siku na hivyo kubakisha lita 28m
kufikia mahitaji ya maji kwa siku.
Akitoa taarifa ya
awali,Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA)
Eng. Aron Joseph kukamilika kwa mradi huu kutaleta manufaa kwa wananchi zaidi
ya 184,642 katika maeneo ya Nkuhungu, Mkonze, Miganga, Chidachi, Michese,Iyumbu,
Mahungu, Ndachi, Njedengwa, Ng’ong’ona, Mlimwa C na Ntyuka kwa
awamu ya kwanza.
Waziri wa Maji Mh. Jumaa
Aweso na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde wakipanda kwenye
tanki la kuhifadhia maji kwa nyakati tofauti kukagua kazi iliyofanyika.
Waziri wa Maji Mh. Jumaa Aweso akiwa amenyoosha mkono kukinga maji yaliyokuwa yakitoka kwenye kisima kilichochimbwa.
0 Maoni