Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Machi 29, 2025 amefanya ukaguzi wa viwanja vitakavyotumiwa kufanyia mazoezi na timu zitakazo shiriki michuano ya CHAN Agosti 2025 na AFCON 2027 kwa Ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda.
Baada ya
ukaguzi huo Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kufanya tathmini ya kazi ya ujenzi
na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwenye michuano hiyo.
Ametoa
maelekezo hayo leo baada ya kupokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
SUMA JKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata ambaye ndiyo wakandarasi wa mradi huo.
Amesema ni
vyema sasa ufuatiliaji wa karibu wa kila hatua za ujenzi na ukarabati
ukafanyika ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa
vifaa vyote ambavyo Mkurugenzi huyo amesema tayari vimenunuliwa na viko Stoo.
"Ndani
ya siku tatu hizi fanyeni tathmini mkutane na Mkandarasi na tembeleeni stoo na
kuhakiki vifaa vyote ambavyo amesema vipo na muwasilishe taarifa kwangu tarehe
1 Aprili 2025.
Mkurugenzi
huyo alimueleza Waziri Mkuu kuwa kwa ujumla ujenzi na ukarabati umefikia
asilimia 80 ya kazi kwa viwanja vyote ambavyo ni pamoja na ujezi wa sehemu ya
kuchezea (pitch) vyumba ya wachezaji (dressing rooms) pamoja na majukwaa.
Mheshimiwa
Majaliwa alikagua viwanja vya Gymkhana, Meja Generali Isamunyo na kiwanja cha
Chuo cha Sheria (Law School) kilichopo Simu 2000 Ubungo.
Michuano ya
CHAN 2025 inayoshirikisha wachezaji wa ndani inatarajiwa kufanyika kuanzia
tarehe 2 hadi 30 Agosti 2025 baada ya kuahirishwa mwaka 2024, Vilevile michuano
ya Afcon inatarajiwa kufanyika mwaka 2027.
0 Maoni