WACHIMBAJI wadogo wa Mgodi wa Dhahabu wa Basia uliopo kijiji
cha Mwanubi Wilaya ya Shinyanga Vijijini wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea huduma ya umeme
katika mgodi huo.
Akizungumza Mwenyekiti wa Mabroka Mkoa wa Shinyanga (CHAMATA)
Masanja Meja amesema kupitia Tume ya Madini imewasaidia kupata miundombinu ya
umeme katika mgodi huo na wameweza kuokoa gharama za uendeshaji kwa zaidi ya
asilimia 70.
“Umeme unatusaidia sana katika uchenjuaji, siku za nyuma kwa
siku tulikuwa tunatumia lita 20 za
dizeli ambayo kwa siku si chini ya shilingi
70,000 kwa mwezi ni Shilingi milioni 2.1 lakini kwa sasa tunatumia umeme
wa Shilingi 15,000 kwa siku kwa mwezi ni Shilingi 450,000 kwetu ni nafuu
kubwa,”amesema Meja.
Aidha, amesema kutokana na miundombinu hiyo ya umeme
uzalishaji umeongezeka kutoka gramu 300 kwa mwezi mpaka gramu 800 hivyo
kuongeza pia mapato ya serikali.
Naye Katibu wa Mgodi wa Basia, Gaga Lupande amesema mgodi
huo umekuwa ukishirikiana na wananchi katika shughuli mbali mbali za maendeleo
ikiwemo uboreshaji wa shule ya msingi Mwanubi pamoja na ujenzi wa Zahanati
unaoendelea.
Amesema kukamilika kwa Zahanati hiyo itaweza kuhudumia Kaya
500 zilizopo katika eneo hilo na kuondoa adha ya wananchi hao kutembea umbali mrefu kufuata
huduma za afya.




0 Maoni