Viongozi mbalimbali wanaoshiriki mkutano wa kimataifa
kuhusu matumizi ya nishati endelevu kwa watu wote (SEforALL) unaofanyika nchini
Barbados wameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili
kuwezesha upatikanaji wa nishati endelevu kwa gharama nafuu.
Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika jijini
Bridgetown, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amesema Tanzania kwa upande wake chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepanga kuwawezesha
asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amesema, kupitia mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere
(JNHPP) unaozalisha megawati 2,115 utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika
na endelevu kwa maendeleo na ustawi wa wananchi katika ngazi mbalimbali.
Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, utekelezaji wa lengo namba 7
katika mpango wa maendeleo ya milenia unahitaji ushirikiano miongoni mwa
Serikali na sekta binafsi katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi ikiwa ni
moja ya utatuzi wa changamoto zilizopo.
Amesema ni muhimu kwa mataifa kuwekeza katika miundombinu
kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi sambamba na kuweka mifumo ya ubunifu
na utashi katika kuwezesha upatikanaji wa nishati kwa usawa bila kuacha makundi
mengine.
Naye, Waziri Mkuu wa Barbados, Mhe. Mia Mottley amesema ni
wakati sasa wa kuweka mkakati wa kimataifa na kukubaliana kushirikiana kumaliza
changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa wote.
Akizungumzia mkutano wa misheni 300 (M300) uliofanyika hivi
karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mia amesema inatia simanzi kuwa na
watu zaidi ya milioni 600 barani Afrika wanaishi bila huduma ya umeme suala
ambalo limesababisha changamoto katika nchi nyingi duniani.
“Tunahitaji kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo, uwe
ufumbuzi wa ndani au kutoka katika nchi yoyote duniani,” amesema Mhe. Mottley.
Kwa upande wake, Rais wa Sierra Leone, Mhe. Julius Maada Bio
amesema katika kipindi hiki ambapo nishati ni nyenzo muhimu katika upatikanaji
wa maendeleo, ni muhimu kuwezesha watu na makundi yote kupata nishati hususani
katika maeneo ya vijijini yanayokabiliwa na umasikini uliokithiri.
“Wanawake na watoto ambao wanatumia muda mwingi kutafuta
nishati ambayo sio safi kwa ajili ya kupikia, wanatakiwa kuwezeshwa kupata
nishati safi na hivyo kutumia muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo,”
ameongeza.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mtendaji
Mkuu SEforALL, Damilola Ogumbiyi, amesema zinahitajika ajenda madhubuti za
kuwezesha kukabiliana na vitendo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo
safi.
“ Tumeshuhudia matokeo yanayosababishwa na ukosefu wa
nishati safi kama vile uharibifu wa mazingira unaosababisha ukame na mafuriko
ambayo kwa kupata nishati safi tunaweza kuondokana nayo,” amesema.
Mkutano huo wa kimataifa ni mwendelezo wa mikutano ya kikanda
na kimataifa inayokusudia kupata suluhisho la changamoto zinazotokana na
matumizi ya nishati chafu.
Mwezi Januari, 2025, viongozi na wakuu wa nchi mbalimbali
barani Afrika na taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya
Maendeleo ya Afrika walikutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta
uwezekano wa kuwawezesha watu takribani milioni 300 barani Afrika kupata huduma
ya nishati ya umeme.




0 Maoni